RC SENDIGA AZINDUA ZAHANATI ILIYOKAMILIKA BAADA YA MIAKA 13
Na. OMM Rukwa
Wananchi wa kijiji cha Ilanga kata ya Muze wilaya ya Sumbawanga wameishukuru Serikali kwa kutoa fedha zilizosaidia kukamilisha mradi wa ujenzi wa zahanati iliyoanza kujengwa mwaka 2009.
Wametoa pongezi hizo jana (08.09.2022) wakati wa halfa ya uzinduzi wa zahanati ya kijiji hicho iliyofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga ambapo Serikali ilitoa shilingi Milioni Sabini na Tano kuikamilisha.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao, Diwani wa Kata ya Muze ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Kalolo Ntira alisema wananchi wamefurahi kuona huduma za afya zikianza kutolewa na kuwa ujenzi ulianza miaka Kumi na Tatu iliyopita kwa nguvu za wananchi.
“Kata ya Muze ina zaidi ya watu 32,000 ikiwa haina kituo cha afya hivyo leo kuanza kutumika wa zahanati ya kijiji cha Ilanga ni mafanikio makubwa .Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutupatia fedha zilizokamilisha mradi huu”alisema Kalolo
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Lightness Msemo alisema Serikali ilitoa shilingi Milioni Sabini na Tano (75,000,000) ili kukamilisha mradi huo na sasa huduma zimeanza kutolewa.
Msemo alisema zahanati hiyi itahudumia wananchi 4,263 wa kijiji cha Ilanga.
Akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga aliwapongeza wananchi wa kijiji cha Ilanga kwa kazi nzuri ya kuanzisha mradi huo kwa kuchangia nguvu na fedha .
Sendiga alisema mradi huo ambao jumla umegharimu shilingi Milioni Mia Moja na Hamsini (150,000,000) itakuwa ni mkombozi kwa wananchi kupata huduma bora za afya karibu.
“Tunao wajibu wa kuifanya zahanati hii iwe kituo cha utoaji huduma bora za afya. Wauguzi mliopo hapa nendeni mkatimize wajibu wenu kuwahudumia wananchi wa Ilanga” alisisitiza Sendiga.
Mwisho
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa