Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Cuthbert Sendiga amezindua Zahanati ya Mpona iliyopo Kata ya Kipeta, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi , amewashukuru wananchi kwa kujitolea nguvu kazi katika ujenzi huo iliyosaidia kwa kiasi kikubwa Zahanati hiyo kukamilika.
Hafla ya uzinduzi wa Zahanati hiyo imefanyika leo tarehe 15 Mei 2023. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amewashukuru na kuwapongeza wananchi kwa kuanzisha ujenzi wa Zahanati hiyo iliyokamilishwa kwa kiasi cha shilingi milioni tisini. Aidha ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kutoa fedha za ukamilishaji .
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Bi Lightness Msemo kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na kuona umuhimu wa kutenga bajeti kwa ajili ya ukamilishaji. Zahanati ya Mpona imepunguza umbali, ambapo awali wananchi walilazimika kutembea umbali wa kilometa kumi na mbili kufuata huduma.
Amewataka wahudumu wa afya katika zahanati hiyo kuhakikisha kuwa wanatoa huduma bora kwa wananchi. Katika hotuba yake Mheshimiwa Sendiga ameitaka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha wanatumia kisima kilichochimbwa na Halmashauri ya Wilaya kuweka kituo cha kuchotea maji (DP) ili kuwasidia wananchi wa Kijiji cha Mpona kupata maji safi na salama kwa matumizi ya nyumbani.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa