CCM YARIDHISHWA MRADI WA MAJI NAMANYERE KUKAMILIKA
Na. OMM Rukwa
Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Rukwa kimeridhishwa na hatua ya serikali kufanikiwa kukamilisha mradi wa maji katika mji wa Namanyele wilaya ya Nkasi ambapo umegharimu shilingi Bilioni 1.3 hadi sasa na utanufaisha wananchi 27,000.
Kauli hiyo imetolewa jana (10.03.2022) na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Rainer Lukala wakati alipoongoza Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Mkoa huo kukagua miradi ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani.
“Tumeridhishwa na jinsi Suwasa ilivyofanikiwa kukamilisha mradi huu ambao utakuwa suluhisho la kero ya maji katika mji wa Namanyere ambapo tumeelezwa kuwa umefikia asilimia 98 .Sasa tuitake serikali kufikisha umeme kwenye eneo hili la chanzo ili maji yaanze kusukumwa kwenda majumbani” alisema Lukala.
Mwenyekiti huyo wa CCM aliongeza kusema changamoto ya miradi ya maji kutokamilika kwa kipindi kilichopangwa lazima sasa ifike mwisho kwa kuwa serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ikitoa fedha kwa wakati.
“Changamoto ya umeme haipaswi kuendelea, Mkuu wa Mkoa (Joseph Mkirikiti) fuatilia Tanesco ili miradi ya maji iweze kuanza kazi mapema na kero ya wananchi kukosa maji safi na salama iishe” aliagiza Lukala.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Sumbawanga (SUWASA) Mhandisi Gibon Nzowa alisema jumla ya shilingi 1,398,289,294/- kati ya shilingi 1,775,096,000/- zimetumika kukamilisha mradi huo wa maji ambao utaongeza uzalishaji maji toka lita 600,000 kwa siku hadi lita 1,800,000 kwa siku.
Mhandisi Nzowa alibainisha kuwa mradi huo umefanikiwa kusambaza bomba kuu lenye urefu wa kilometa 3.9 na umesambaza mabomba ya maji yenye urefu wa kilometa 6.5 katika mji wa Namanyere.
Mhandisi Nzowa aliwaeleza wajumbe hao kuwa kazi inayosubiriwa kwa sasa ni TANESCO kufikisha umeme katika mtambo wa kusukuma maji ili wananchi waanze kupata huduma.
Katika hatua nyingine Kamati hiyo ya Siasa ya CCM mkoa ilikagua pia mradi wa maji kijiji cha Katongolo wilaya ya Nkasi ambao unatekelezwa na Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) na tayari umegharimu shilingi 202,518,074/- kati ya shilingi 349,732,107/- na umefikia asilimia 80.
Meneja wa Ruwasa Nkasi Mhandisi Shafii Shabani alisema mradi huo utanufaisha wananchi 2,734 wa kijiji cha Katongolo huku akitaja changamoto ya umeme kukwamisha zoezi la majaribio ya kusambaza maji kwenye vituo vya kuchotea (BP) 14 zilizojengwa.
Akijibu hoja za tatizo la umeme kukwamisha miradi hiyo kuanza kazi, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ameahidi kulifuatilia na kuchukua hatua za haraka ili Tanesco wafikishe huduma hiyo.
Pamoja na miradi ya maji, Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Rukwa imekagua pia mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya kata ya Paramawe itakayogharimu shilingi Milioni 470 ambayo ujenzi wake utakamilika Juni mwaka huu.
Kamati hiyo ya Siasa imemaliza ziara wilaya ya Nkasi na wiki ijayo itaendelea na ziara ya ukaguzi wa miradi katika wilaya ya Kalambo.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa