Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Mhandisi Atashasta Nditiye ametoa habari nzuri kwa wana Rukwa na mikoa yote iliyopo pembezoni mwa ziwa Tanganyika juu ya ujio wa meli mpya ambayo itaanza kutengenezwa baada ya kusainiwa kwa mkataba mwezi wa tatu mwaka huu.
Amesema kuwa mwambao huo umekuwa ukitegemea meli moja tu ya MV Liemba mbayo ina miaka zaidi ya 100 ikitoa huduma katika ziwa hilo na kukiri kuwa ikipatikana meli hiyo ya pili changamoto ya usafiri kwa abiria na mizigo itapungua.
“Mkataba Utasainiwa mwezi wa tatu ili meli hiyo iweze kuhudumia watanzania walioko mwambao wa ziwa Tanzanganyika sasa tunatumia meli moja tu ya MV Liemba, kwakweli kabisa ni meli ya siku nyingi in miaka zaidi ya 100 ikiwa inafanya kazi katika ziwa Tanganyika, kwahiyo tukiipata hiyo nyingine zikawa mbili, ninahakika kabisa changamoto za usafiri wa abiria na mizigo utakuwa umepungua,” Alimalizia.
Ameyasema hayo alipoongea na waandishi wa habari alipotembelea bandari ya Kasanga ili kujionea mandeleo na changamoto za bandari hiyo ambayo ndani ya miaka mitatu imeiingizia Tanzania shilingi Bilioni 2.2 huku ikisafirisha mizigo na abiria ndani na nje ya nchi kama vile DR Congo na Burundi.
Kwa upande wake afisa wa bandari hiyo Suleiman Kalugendo ameiomba serikali kujitahidi kufanya upanuzi wa gati ya bandari hiyo yenye urefu wa mita 20 na badala yake ifikie walau mita 120 ili kuweza kuhudumia meli za mizigo na abiria kwa wakati mmoja kwani meli ya MV liemba peke yake ina urefu wa mita 70 hivyo hupata changamoto pindi meli mbili zinapotaka kutia nanga.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa