Kumekuwa na wimbi la kusafirisha na kuhamisha mifugo ya kufuga bila kufuata taratibu kutoka eneo moja hadi jingine jambo ambalo linazua migogoro baina ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi na kusababisha uharibifu wa mazingira na ueneaji wa magonjwa ya mifugo. Serikali ilikwishatoa Tamko la utaratibu wa kuhamisha mifugo ya kufuga kutoka sehemu moja hadi nyingine, mwaka 2006.
Vile vile Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2002 nao unakataza kabisa uswagaji holela wa mifugo katika maeneo yaliyo na barabara za lami, njia za reli au njia za maji na unawataka Wakuu wa Wilaya kulisimamia Agizo hilo.
Kwa kuzingatia maagizo ya Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2002, Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya mwaka 2003 na Kanuni zake na Utaratibu kutoa vibali vya kusafirisha mifugo ya kufuga kutoka sehemu moja hadi nyingine ulitolewa ‘Taarifa kwa Umma’ mwaka 2006 na Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo.
Mkoa unatoa maelekezo yafuatayo:-
1. Mifugo kwa ajili ya kufuga isihamishwe kutoka katika Kijiji ama Wilaya ama Mkoa kabla ya kupata Idhini/Kibali cha Kijiji, Wilaya ama Mkoa inakopelekwa.
Hivyo inapaswa Kijiji, Wilaya na Mkoa itoe kwanza idhini ya kupokea mifugo hiyo ya kufuga ndipo kibali cha kusafirisha mifugo (Animal Health Livestock Movement Permit) kitolewe kwa mujibu wa Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2007 (GN no.28), mwaka 2013 (GN no.225) na mwaka 2018 (GN no.475).
2. Kwa mujibu wa Utaratibu wa Serikali uliotolewa - Vijiji, Wilaya na Mikoa inapaswa isitoe Vibali vya kupokea mifugo ya kufuga kabla ya kujiridhisha kwamba wanayo maeneo ya kutosha ya malisho ya mifugo yaliyopimwa na kuthibitishwa na Wataalam kama yanafaa kwa malisho na yana maji ya kutosha.
3. Madaktari wa Mifugo wa Wilaya ndio wenye dhamana kisheria kutoa Vibali ‘Animal Health Livestock Movement Permit’ vya kusafirisha mifugo, na wanafanya hivyo kudhibiti ueneaji wa magonjwa ya mifugo nchini.
4. Kabla ya kutoa Vibali vya kusafirisha mifugo (Animal Health Livestock Movement Permit), Madaktari wa Mifugo wa Wilaya ama Wawakilishi wao waidhinishwa wahakikishe kwamba mifugo imeogeshwa na imechanjwa chanjo za kuzuia magonjwa husika kabla ya kuiruhusu mifugo hiyo kusafirishwa ili kuzuia uenezaji wa Magonjwa ya Mifugo.
5. Mifugo isafirishwe kwa njia isiyoharibu mazingira na miundombinu mingine kama ilivyoainishwa kwenye Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2002, Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya mwaka 2003 na Kanuni zake.
(a) Kama mifugo inasafirishwa ndani ya maeneo ya Wilaya inapaswa kufuata njia rasmi za kupitisha mifugo zinazotambulika (Official stock-routes).
(b) Kama mifugo inasafirishwa kwenda nje ya Wilaya, Mkoa ama inatoka kwenye Minada ya Awali (Primary Livestock Markets) kwenda maeneo mengine ya ufugaji au Minada ya Upili/Mpakani (Secondary/Border Livestock Markets) inapaswa ipakiwe na kusafirishwa kwenye malori.
6. Ni jukumu la kila Halmashauri kuhakikisha kuwa inajenga na kutumia miundombinu ya kuwezesha mifugo kupakiwa na kushushwa kwenye magari pamoja njia rasmi za kupitisha mifugo zinazotambulika (Official stock-routes).
7. Usafirishaji wa Wanyama unapaswa kuzingatia pia matakwa ya Sheria ya Ustawi wa Wanyama Na.19 ya mwaka 2008 na Kanuni zake. Pamoja na Sheria nyingine za nchi, Kanuni na Miongozo mbalimbali iliyowekwa na Serikali.
Wilaya zinashauriwa zisimamie maelekezo haya kikamilifu na hatua za kinidhamu na kisheria zichukuliwe kwa Daktari/Mtaalamu wa Mifugo, Kiongozi wa Serikali ama Mfugaji yeyote atakayekiuka utaratibu huu.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa