Hali ya Kilimo katika Mkoa.
Kilimo ndiyo shughuli kuu ya kiuchumi na inayoajiri watu wengi katika Mkoa wa Rukwa. Kwa miaka mingi Kilimo kinatupatia chakula cha kutosheleza mahitaji yetu na kuwa na ziada ambayo huuzwa kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula na wanunuzi wengine ndani na nje ya Mkoa wetu.
Mkoa una eneo la hekta 1, 660,600 zinazofaa kwa kilimo kati ya hizo eneo lililolimwa katika msimu wa Mwaka 2022/2023 ni hekta 564,335.3 sawa na asilimia 34 ya eneo lote linalofaa kwa Kilimo.
Mazao yanayolimwa kwa wingi katika Mkoa huu ni pamoja na Mahindi, Mpunga, Ulezi, Alizeti, Maharage, Ngano, Mtama na Muhogo. Tija ya mazao haya bado ni ndogo ikilinganishwa na ile iliyofanyiwa utafiti katika mazingira ya wakulima. Sababu zinazochangia kuzalisha kwa tija ndogo ni matumizi kidogo ya pembejeo za kisasa, zana duni za kilimo, kilimo kinachotegemea mvua na uzalishaji usiokuwa wa kibiashara.
Katika msimu wa kilimo wa 2022/2023 Mkoa ulilenga kulima jumla ya hekta 606,589.20 za mazao mbalimbali ya chakula na biashara na kulenga kuvuna jumla ya tani 1,582,287.62 za mazao ya chakula na biashara.
Katika utekelezaji zililimwa hekta 498,012.5 za mazao ya chakula na hekta 66,323 za mazao ya biashara na kufanya jumla ya hekta 564,335.3. sawa na asilimia 93 ya malengo. Aidha, mavuno yalikuwa ni kiasi cha tani 1,469,716.83 za mazao ya chakula na tani 109,534.85 za mazao ya biashara hivyo kufanya jumla ya uzalishaji wa mazao yote (chakula na biashara) kuwa ni tani 1,579,251.7.
Uzalishaji wa Mahindi kwa Mwaka 2022/2023
Mahindi ni zao kuu la chakula na biashara katika Mkoa. Zao hili hulimwa karibia na wakulima wote wanajishughulisha na kilimo cha mazao. Katika msimu wa kilimo wa 2022/2023 jumla ya hekta 246,031.50 zililimwa zao la mahindi. Eneo hilo ni sawa na asilimia 49.4 ya eneo lilolimwa mazao ya chakula. Uzalishaji wa mahindi katika msimu huo wa 2022/2023 ulikuwa ni tani 803,414.40 sawa na asilimia 54.7 ya uzalishaji wa mazao ya chakula.
Mahitaji ya chakula kwa Mkoa wa Rukwa kwa Mwaka 2023/2024 kwa watu 1,540,519 ni jumla ya tani 506,060.49 ikiwa ni tani 365,488.13 za mazao jamii ya wanga na tani 140,572.36 za mazao jamii ya mikunde; hivyo kuwa na ziada ya tani 716,302.56.
Matarajio yetu ni kwamba katika kipindi cha Mwaka 2023/2024 eneo la jumla ya hekta 620,578.5 za mazao mbalimbali litalimwa. Kati ya eneo hilo hekta 557,404.75 ni kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula, hekta 63,173.75 ni kwa ajili ya kilimo cha mazao ya biashara. Jumla ya tani 1,762,337.15 za mazao zinategemewa kuzalishwa. Kati ya kiasi hicho tani 1,654,840 ni za mazao ya chakula, tani 107,497.15 za mazao ya biashara.
Katika Msimu 2023/2024 Serikali imeendelea kutoa Ruzuku ya Mbolea ili kuwasaidia wakulima kuzalisha kwa tija na kupunguza gharama za uzalishaji. Mahitaji ya mbolea katika Mkoa kwa msimu wa Kilimo 2023/2024 ni Tani 38,135.
Mkoa umeweka msukumo katika mazao mengine ya kimkakati yatakayopelekea kukua kwa biashara ya mazao katika Mkoa. Mazao yaliyopewa kipaumbele ni Kahawa, korosho na Alizeti. Katika msimu 2016/2017 Mkoa ulianza juhudi za kufufua zao la Kahawa. Hadi sasa jumla ya miche 135,981 ya kahawa imepandwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa. Katika msimu huu 2022/2023 jumla ya miche 27,460 ya Kahawa imepandwa lakini bado haijaanza kuzaa.Katika zao la korosho hadi sasa kuna jumla ya miche 14,109 imepandwa na inaendelea vizuri haijaanza kutoa uzalishaji, zao la parachichi kuna mashamba darasa mawili yenye jumla ya miche 188 yameanzishwa katika kijiji cha kichema na mtipe Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga na pia kuna jumla ya miche 2,420 ambayo imepandwa na wakulima mbalimnbali.
Zao la alizeti katika msimu huu 2022/2023 Mkoa ulilima jumla ya hekta 61,022 ambazo zimezalisha tani 68,699.01. Kwa zao la michikichi katika msimu wa 2022/2023 jumla ya miche 10,580 imegawiwa kwa wakulima katika Halmashauri ya wilaya ya Kalambo na Nkasi na jumla ya mbegu 20,000 imepandwa katika kitalu cha chini katika Halmashauri ya wilaya ya Kalambo ambapo miche itagawiwa kwa wakulima katika msimu wa 2023/2024.
Ununuzi wa Mahindi kupitia NFRA.
Katika Msimu wa 2023/2024 Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula walipangiwa kununua tani 20,000 hadi sasa wameshanunua kiasi cha tani 35,000. Bei ya kununualia ni shilingi 900 kwa kilo kwa vituo vya Laela, Mazwi, na katika vihenge (maghala mapya) ya Kanondo na shilingi 800 kwa kilo kwa vituo vya Nkasi na Kalambo.
Kilimo cha umwagiliaji
Mkoa wa Rukwa una jumla ya Skimu za Umwagiliaji 58 zenye ukubwa wa Hekta 67,401 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji hata hivyo juhudi za kuendelea kuyatambua maeneo yote yanayofaa kwa umwagiliaji zinaendelea. Skimu 6 kati ya 58 sawa na hekta 7250 ambayo ni 8.6% ya eneo lote linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji zimeendelezwa kwa kujengewa miundombinu bora ya Umwagiliaji. Skimu hizo ni pamoja na Sakalilo, Katuka, Ng’ongo, Singiwe, Katongolo/Lwafi na Ulumi.
Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Mkoa unatekeleza ujenzi wa skimu ya umwagiliaji wa Ilemba yenye ukubwa wa hekta 1,650 ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu yote ya mashambani. Hadi sasa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ipo katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi. Pia, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kupima na kufanya usanifu wa kina skimu ya Lwafi-katongolo(Nkasi DC) yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 3,200. Aidha, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kupima na kufanya usanifu wa kina wa skimu ya Umwagiliaji ya Legezamwendo(Kalambo DC) yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 5,500.
Hali ya Vyama vya Ushirika katika Mkoa wa Rukwa
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa