MKUU wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa Mh.Said Mtanda ametoa siku saba kwa wanafunzi wote 1,641 kujiunga Kidato cha Kwanza katika shule walizopangiwa.
Alisisitiza kuwa Walimu Wakuu wawapokee wanafunzi hao hata kama hawana sare za shule na kutembea peku .
"Wabunge,madiwani,wataalamu,maofisa elimu kata, maofisa tarafa,watendaji wa vijiji na kata pia Ofisa Elimu Elimu ya Msingi Wilaya wahakikishe wazazi na walezi watoto wao wanaripoti shuleni kwa wakati vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao" alieleza.
Alisema wanafunzi hao 1,641 ambapo hawajajiunga na Kidato cha Kwanza katika shule walizopangiwa wilayani humo tangu zifunguliwe Januari 11,mwaka huu ni sawa na asilimia 40 ya wanafunzi 4,301 waliochaguliwa.
Mtanda alitoa maelekezo hayo alipokutana na wanahabari na kuzungumzia kufunguliwa kwa shule za msingi na sekondari na wanafunzi walioripoti Kidato cha Kwanza wilayani humo.
"Wanafunzi hao 1,641 kabla ya mwisho wa siku hii wawe wameripoti katika shule walizopangiwa ili waajiriwe katika mfumo ambao una muda maalumu...
Serikali imeelekeza wanafunzi wanaojiunga Kidato cha Kwanza wote wasajiliwe katika mfumo......
Katika wilaya hii kati ya wanafunzi 4,301 waliochaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza wanafunzi 2,660 sawa na asilimia 60 wameripoti katika shule walizopangiwa na 2,582 wamesajiliwa katika mfumo"alieleza.
Kuhusu miundombinu ya vyumba vya madarasa amesema wilaya hiyo haina changamoto ya upungufu wake kwa kuwa mwaka uliopita maboma 560 ya shule za msingi na sekondari ujenzi wake ulikamilika.
Kwa upande wa samani alisema kuwa wilaya hiyo ilikuwa na upungufu wa madawati,viti na meza 5,621.
"Ili kukabiliana na upungufu huo viti 473 na meza 516 vilivyokuwa vimeharibika,vimekarabatiwa na kusambazwa katika shule 28 za sekondari pia kila shule ya sekondari imeelekezwa kutengeneza viti na meza 20"alisema.
Akiongeza kuwa " Miti iliyoanzishwa wakati wa ukarabati wa barabara ya Wampembe imechanwa na zimepatikana mbao 650 ambapo vimetengenezwa viti na meza 500 na kusambazwa katika shule zenye mahitaji" alibainisha.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa