.
Hali ya usalama imerejea katika Kata ya Kabwe Wilayani Nkasi baada ya kushuhudiwa kwa hali ya vurugu na uharibifu wa mali siku ya Jumatatu ya tarehe 11 Septemba 2023.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere amewataka wananchi wa Kata ya Kabwe kuendelea na shughuli za uzalishaji mali kama kawaida kwa kuwa Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi.
Ameyasema hayo Leo Septemba 12, 2023 alipofanya ziara ya ukaguzi katika Kata ya Kabwe. Awali zilijitokeza vurugu na uharibifu wa mali zilizotokana na hatua za Serikali kukidhibiti kikundi cha watu wanaopiga ramli chonganishi
wanaojulikana kama Kamchape au Lambalamba.
Mheshimiwa Makongoro amekemea vikali vitendo vya uharibifu wa mali, wizi na vurugu vilivyofanywa na wananchi hao huku akieleza kuwa kilichofanyika ni uhalifu usiopaswa kufumbiwa macho na unaotakiwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Amelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha wahusika wote wanafikishwa Mahakamani kwa uhalifu huku akilipongeza Jeshi la Polisi kwa kuchukua hatua kwa wakati kudhibiti uhalifu huo kwa kushirikiana na raia wema.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amewataka wananchi Mkoani Rukwa kuhakikisha kuwa hawatoi nafasi ya kurubuniwa na kuchonganishwa kwa ramli chonganishi za Lambalamba. Amesema kikundi hicho kinatumia fursa ya kuaminika na jamii kujipatia fedha.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa