Mkuu wa mkoa wa Rukwa h. Joachim Wangabo amewataka viongozi na watendaji wa serikali katika ngazi mbalimbali pamoja na wadau wa lishe mkoani humo kuonyesha bayana michango wao katika kukabiliana na tatizo la utapiamlo, kubaini kiwango cha utapiamlo katika maeneo yao na kutoa taarifa na tathmini ya ufanisi wa zoezi hilo.
Amesema kuwa inasikitisha sana kuona mkoa wa Rukwa ukiwa ni miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini, ukiwa na asilimia 56.3 ya watoto wa umri wa miaka mitano wenye udumavu tofauti na wastani wa kitaifa wa asilimia 34 na kushtushwa zaidi na asilimia 23 ya watoto hao kuwa na uzito pungufu ikilinganishwa na asilimia 13.6 ya kitaifa.
Ameyasema hayo katika hotuba yake ya uzinduzi wa mpango mkakati wa lishe wa mkoa ulioshirikisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, waganga wakuu na timu zao za afya, maafisa maendeleo ya jamii, wachumi wa halamashauri, wataalamu kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa pamoja na kamati ya ulinzi na usalama Mkoa.
Aidha, ametaja sababu kadhaa zinazosababisha hali hiyo kuwa ni pamoja na ulishaji duni wa watoto wachanga na watoto wadogo, ukosefu wa elimu ya lishe kwa sehemu kubwa ya jamii, ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi, uwekezaji mdogo katika masuala ya lishe, pamoja na kutopanga uzazi.
Mh. Wangabo alisema kuwa watoto waliopata huduma bora za lishe hasa katika kipindi cha siku 1,000 za kwanza za uhai wao, yaani tangu mama anapopata ujauzito hadi mtoto anapotimiza umri wa miaka miwili wanapata faida zitakazodumu katika maisha yao yote.
“Faida apatazo mtoto ni pamoja na ukuaji na maendeleo mazuri ya ubongo uwezo mzuri wa kukabiliana na maradhi, uwezo mzuri kiakili, uwezo wa kujifunza na ufanisi mzuri masomoni, uwezo zaidi wa kujiingizia kipato wakati wa utu uzima. Lishe duni si tu inaathiri maendeleo ya ukuaji wa watoto wetu kimwili na kiakili bali pia ni chanzo cha kupungua kwa tija katika nguvu kazi ya taifa.”Alisema.
Kwa upande wake mratibu wa Afya ya mama na mtoto mkoa wa Rukwa Asha Izina alisema kuwa lengo kubwa ni kufanikisha suala la kuboresha hali ya lishe na kupunguza athari za utapiamlo katika kila Wilaya ambapo Mkuu wa wilaya husika atatkiwa asimamie hilo.
‘’Malengo ni kuhakikisha kuwa Wilaya inasimamia ipasavyo utekelezaji wa afua za lishe
Kuchukua hatua madhubuti za kupunguza hali duni ya lishe katika eneo lake
Kupanga na kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza afua za lishe katika mipango ya Halmashauri, ‘’ alisema
Mkoa wa Rukwa ni 17% tu ya watoto wa umri wa chini ya miezi sita ndio wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee kama inavyosauriwa na wataalamu. Pia 32.8% ya watoto wenye umri wa miezi 6-23 ndiyo waonapata chakula mchanganyiko unaostahili, halikadhalika 40.9% ya watoto wa miezi 6-23 wanapata idadi ya milo mitano inayotakiwa kwa siku. 12% ya watoto wa miezi 6-23 wanapata kiwango cha chini cha mlo unaokubalika kama ilivyoainishwa na vigezo vya shirika la afya Duniani.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa