Waziri wa Kilimo Mh. Japhet Hasunga ameagiza kukamatwa kwa Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Rukwa Anosisye Mbetwa pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya kusambaza pembejeo ELI AGROVENT CO. Elias Ndomba kwa kushirikiana kuingia mkataba kinyume na taratibu za serikali hali iliyopelekea chama kikuu cha ushirika mkoani humo Ufipa Cooperative Union (UCU) kutapeliwa shilingi Milioni 277 huku wanachama wake wakiendelea kuhangaika juu ya upatikanaji wa mbolea.
Miongoni mwa vipengele vya Mkataba huo wa miaka mitatu ulioingiwa tarehe 22.11.2019 vinasema kuwa Kampuni hiyo itamuuzia UCU mbolea ya tani 1,901.05 yenye thamani ya shilingi Bilioni 2,384,266,812 ambapo chama kinatakiwa kilipe asilimia 30 amabayo ni sawa na Shuilingi 715,280,064 na huku msambazaji huyo akimalizia kulipa asilimia 70 na kuwapa wakulima hao mbolea na kutaka kulipwa fedha yote kamili kufikia tarehe 30.4.2020
Aidha, Kipengele cha 9 cha mkataba huo unaonesha kuwa malipo hayo yanasimamiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa asilimia 100 jambo ambalo Ofisi ya Mkoa haifahamu na zaidi ya hapo bei ya mbolea iliyoorodheshwa kwenye mkataba huo iko juu ukilinganisha na bei elekezi ya serikali kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020 ikionesha kuwa wakati katika Manispaa ya Sumbawanga bei ya mfuko wa Kilo 50 wa mbolea ya kupandia DAP ukiuzwa shilingi 60,708 na mbolea ya kukuzia UREA shilingi 57,021 Kampuni hiyo itauza DAP shilingi 65,086 wakati UREA itauza shilingi 62,320.
Mh. Hasunga alisema kuwa lengo la kuanzisha vyama vikuu vya ushirika katika mikoa ni kuweza kusaidia kuagiza pembejeo kwa niaba ya wanachama ili gharama za mbolea na hivyo kuushangaa mkoa wa Rukwa kwa kukubali kuingia mkataba wa kuuziwa mbolea ambayo bei yake ipo juu na kufafanua kuwa bei kubwa ya mbolea inatokana na gharama za usafirishaji gharama za faida kutoka bandarini kuja huku na kuongeza kuwa kuona manufaa ya ushirika bei ya ushirika inatakiwa iwe chini ya bei za soko ambazo wanauza wafanyabiashara kwenye masoko.
“Haitakiwi kuzidi, Ikizidi mnakuwa mmedukuliwa, mmelanguliwa, mmeibiwa,mmedhulumiwa, hivyo basi kwa muktadha huo agizo langu la tatu viongozi wote waliohusika kuingia mikataba mibovu kwa kisingizio kwamba serikali ndio imeagiza kuanzia sasa watakuwa chini ya ulinzi na kwa kuanzia naagiza Afisa ushirika Mrajis Msaidizi wa Mkoa, chini ya Ulinzi kuanzia muda huu, wa pili Muuzaji wa Pembejeo aliyeingia mikataba kinyume na serikali, akawatapeli wakulima akasema mukilipa yeye atawapa asilimia 70 hajawapa msimu wa kilimo umeanza, mpaka tunapanda hatuna mbolea, mpaka muda huu hatuna mbolea yuko chini ya ulinzi, hatuwezi kuwa na viongozi wa namna hiyo wanahujumu uchumi , wanawanyayasa wakulima halafu watu wanasema ni serikali, serikali imeagiza wafanye hayo?” Alisema.
Na kuongeza kuwa Mrajis huyo ashushwe cheo hata kama atashinda kesi yake hiyo kwani serikali haiwezi kuwavumilia watu wanaokwamisha juhudi za serikali katika kuwakomboa wakulima na kuwaagiza vuiongozi wa vyama vyote vya ushirika kuwa na Takwimu sahihi za wanachama, maeneo wanayolima na shughuli wanazozifanya na kuhakikisha kila chama kinakuwa na daftari ili watakapotembelewa na kiongozi wa serikali daftari la wanachama liwe ndio jambo la kwanza kuliwasilisha.
“Cha Kwanza kunionyesha ni daftari la Wanachama, tumkute kwa jina, tumkute kwa namba ya simu, tumkute na anuani yake, tumkute na mazao anayolima na alichochangia kwenye chama, hisa zake na kama ni akiba tuzikute, zionekane kwenye daftari la kudumu, kinyume cha hapo chama chochote kitakuwa kimekiuka taratibu tunataka takwimu ziwe sahihi,” Alisisitiza.
Pia Mh. Hasunga alisema kuwa ukaguzi uliofanywa na shirika la Ukaguzi la vyama vya Ushirika nchini (COASCO) unaonesha kuwa vyama 5 tu kati ya 80 ndivyo vilipata hati ya kuridhisha, huku vyama 65 vikiwa na hati za mashaka, vyama 15 vikiwa na hati zisizoridhisha, na vyama 5 vikiwa na hati chafu na kuongeza kuwa vyama hivyo vilivyopata hati ya kuridhisha haimaanishi kuwa ni visafi na kuwataka viongozi wa vyama hivyo kujirekebisha
Ametoa maagizo hayo jana ijumaa 27.12.2019 alipokuwa akizungumza na vyama vya Ushirika (AMCOS) kutoka katika Halmashauri nne za Mkoa wa Rukwa katika mkutano uliofanyika katika ukumbu wa ofisi ya Mkuu wa mkoa huo mjini Sumbawanga.
Wakati wakiwasilisha malalamiko hayo Mwenyekiti wa Chama cha Siruri AMCOS Adam Msangi kutoka wilayani Kalmabo alisema kuwa chama chake kilichangia shilingi 19,450,000 na kupewa mbolea ya kupandia aina ya DAP mifuko 200 ambayo haikuweza kukidhi mahitaji ya wanachama wa AMCOS hiyo.
“Ilitokea sintofahamu kati ya chama kikuu pamoja na mrajis ambaye ni wakilishi wetu upande wa serikali ambaye ametupelekea sisi mazao mpaka sasa yako taabani, hayana mwelekeo wowote katika suala la mbolea, napenda nikuhakikishie ndugu waziri kwamba, hjata hivyo vyama ulivyoahidiwa hapa kwamba wameshapata DAP sio kweli ,” Alisema
Naye Geofrey Senga mwenyekiti wa Luwa AMCOS alisema kuwa kilichokosewa kwenye mkataba ni kuwa msambazaji alisema kuwa ataleta mbolea tani 450 na UCU imuwekee shilingi 715,280,064 ikaonekana chama chetu kikuu kilimuingizia msambazaji shilingi milioni 277 kabla ya msambazaji huyo kuleta zile tani 450.
“Walimuingizia kama shilingi milioni 277 na inaonekna yeye hana uwezo wa kutuongezea ile iliyoahidi asilimia 70 ili atupatie pembejeo na kinachoonekana sina uhakika sana alichukua zile milioni 277 akenda kwa IKUWO (msambazaji wa pembejeo) akanunua mbolea shilingi 55,000 akawawa ametupiga mbolea shilingi 10,000 ana milioni 44 amabzo ameshaweza mfukoni,” Alisema.
Mkoa wa Rukwa una vyama 74 vya Mazao na Masoko (AMCOS) huku chama hicho kikuu cha ushirika kikiwa na wanachama 58 ambao wameekeza fedha zao kwenye chama kikuu kwaajili ya kujipatia mbolea kwaajili ya msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa