Jukwaa la Ngano Rukwa (JUNGARU) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Uyole Mkoani Mbeya wamefanya Mkutano na wadau wa zao la ngano Mkoa humo ukiwa na lengo la kujadili na kuinua Kilimo cha zao hilo ili kuweza kumkomboa mkulima kwani soko la zao hilo ni kubwa ndani na nje ya nchi ukilinganisha na zao la mahindi ambapo wakulima wengi wamekuwa wakilima nakukosa soko la uhakika.
Katika Kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa mkutano huo uliambatana na uzinduzi wa wa mradi wa Kilimo cha ngano uitwao Technologies for African Agriculture Transformation (TAAT) wenye lengo la kuunga mkono na kuhakisha Kilimo cha ngano ndani ya mkoa kinakuwa chenye tija ili kusaidia kuongeza wigo wa mazao ya biashara.
Mkuu wa Mkoa wa rukwa Mh. Joachim Wangabo ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mkutano huo alisema kuwa Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa inayozalisha kwa wingi zao la mahindi na kuongeza kuwa imefika wakati sasa kuwahimiza wakulima hao kulima zaidi mazao ya kibiashara ikiwemo zao la alizeti, kahawa na ngano.
“Mradi huu ambao lengo lake ni kuongeza tija katika uzalishaji wa ngano hadi kufikia tani 3.5 kwa hekta moja, hii inaonyesha ni jinsi gani serikali yetu kupitia taasisi hii inadhamira ya dhati kuhakikisha kuwa kilimo cha ngano kinakuwa cha tija katika soko letu, mahitaji ya ngano ni makubwa kufikia tani 1,000,000 ambapo kwa sasa uzalishaji ni tani 100,000 tu, hivyo ongezeko la uzalishaji litasaidia serikali kupunguza matumizi ya fedha nyingi za kigeni kuagiza ngano nje ya nchi,” Alibainisha.
Akishukuru ushirikiano anaoupata kutoka katika ofisi ya mkuu wa mkoa Mwenyekiti wa JUNGARU Mama Mzindakaya alisema kuwa ushauri alioupata kutoka kwa Mh. Wangabo wa kusajili jukwaa hilo na kuwa chama cha ushirika wamelifanyia katika na hivyo wapo katika hatua za mwisho ili kuweza kukamiliza usajili katika wizara ya mambo ya ndani na kuongeza kuwa zao la ngano ni moja ya mazao rahisi kuyalima.
Wakati akiutambulisha mradi huo mratibu wa mradi huo kutoka Ethiopia Solomon alisema kuwa bara la afrika linatumia pesa nyingi sana katika kuagiza chakula kutoka nje ya afrika na hivyo imefika wakati sasa waafrika kuanza kujitegemea katika kuzalisha chakula cha kutosha na hatimae kuweza kutumia fedha hizo kwa maendeleo mengine.
Katika Mkutano huo maazimio yaliyofikiwa ni pamoja na Kila Wilaya kuwa na wakulima wa ngano wasiopungua 300 kufikia tar 30 Desemba, 2018. Wakulima wa ngano wachange fedha kwa ajili ya kununua Mbegu kulingana na uhitaji wake ili ikanunuliwe Uyole Mbeya kufikia 30 Desemba, 2018. Mradi wa TAAT kufanya mafunzo ya Kilimo bora cha ngano kwa wakulima wa ngano kila Wilaya, mafunzo yatahusu pia ujasiriamali, pamoja na ushirika
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa