Sekta ya Elimu
Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kila Mtoto anayestahili kupata Elimu Msingi (Basic Education) anapata Elimu hiyo. Mpango wa Serikali wa Elimu Msingi bila malipo umekuwa na mafanikio makubwa. Mafanikio hayo ni pamoja na;-
Mafanikio Kitaaluma:
Matokeo ya Mitihani Mwaka 2017/2018
Mkoa umeendelea kusimamia suala la Elimu kikamilifu. Aidha, katika upimaji wa Mitihani ya kitaifa matokeo ya ufaulu yamekuwa yakiongezeka kama ifuatavyo;
Matokeo ya mtihani wa upimaji kwa Darasa la Nne yameendelea kuimarika kutoka ufaulu wa aslimia 88.00 kwa mwaka 2016 hadi asilimia 89.11 kwa mwaka 2017 .
Matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi yanaonesha kupanda kwa ufaulu wa wanafunzi kutoka ufaulu wa 66% kwa mwaka 2016 hadi 68.05% kwa mwaka 2017. Kulingana na Tathmini ya mtihani wa utimilifu ufaulu unatarajia kuongezeka hadi kufikia asilimia 78% kwa mwaka 2018.
Idadi ya Wanafunzi waliofaulu 12,867 wote walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2018. Kati yao Wanafunzi 54 shule za bweni na 12,813 shule za kutwa. Wanafunzi hao wote walipatiwa nafasi za kuendelea na masomo.
Katika mtihani wa upimaji Kidato cha Pili mwaka, 2017, ufaulu wa wanafunzi uliongezeka kutoka asilimia 87.6 mwaka 2016 hadi asilimia 92.08 kwa mwaka 2017.
Matokeo ya mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2016, Mkoa ulishika nafasi ya 12 kitaifa kati ya Mikoa 31 ukilinganisha na mwaka 2017 ambapo Mkoa ulishika nafasi ya 13. Aidha Jitihada za ufundishaji, ufuatiliaji na usimamizi zimefanyika ili kwa mwaka 2018 Mkoa uwe katika nafasi nzuri zaidi kitaifa.
Matokeo ya mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2017 Mkoa ulishika nafasi ya 8 kitaifa kati ya Mikoa 29 ukilinganisha na mwaka 2018 ambapo Mkoa ulishika nafasi ya 13. Aidha, jitihada za ufundishaji, ufuatiliaji na usimamizi zinaendelea kufanyika ili kwa mwaka 2019 Mkoa uweze kushika nafasi nzuri zaidi kitaifa ukilinganisha na mwaka huu.
Utekelezaji wa miundombinu ya elimu Mkoa
Katika kipindi cha mwaka 2015 tulikuwa na maabara 24, na kwa mwaka 2018 maabara zimeongezeka hadi kufikia maabara 31. Aidha, maabara 177 zinaendelea kujengwa katika Mkoa wetu ambazo zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Katika kipindi cha mwaka 2015 Vyumba vya madarasa vilivyokuwepo kwa shule za msingi na Sekondari ni 3,140 na kwa mwaka huu wa 2018 vyumba vya madarasa vimeongezeka hadi kufikia 3,329.
Katika kipindi cha mwaka 2015 nyumba za walimu wa shule za msingi na Sekondari zilikuwa ni 1,955 na kwa mwaka 2018 zimeongezeka hadi kufikia nyumba 2,124.Ongezeko hili ni jitihada za serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu kwa walimu.
Katika kipindi cha mwaka 2015 matundu ya vyoo yalikuwepo ni 4,391 na kufikia mwaka 2018 matundu ya vyoo yameongezeka kufikia 5,438.
Serikali imeendelea na jitihada za kuboresha sekta ya elimu kwa kuhakikisha madawati yanatengenezwa mashuleni. Aidha, katika kipindi cha mwaka 2015/2016 tulikuwa na madawati 37,311 kwa shule za msingi, meza 21,757 na viti 22,093 kwa shule za Sekondari. Aidha, kwa mwaka 2018 madawati yameongezeka kufikia 80,501 kwa shule za msingi, meza na viti 33,686 kwa sekondari kufikia mwaka huu 2018.
Ujenzi wa chuo cha VETA Sumbawanga
Tarehe 31/08/2018 VETA Makao Makuu Dar es Salaam, VETA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mbeya pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa tulifanya hafla fupi ya kumkabidhi Mkandarasi TENDER INTERNATIONAL kiwanja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Chuo Cha Ufundi Stadi (VETA) katika Manispaa ya Sumbawanga pamoja na Mkandarasi, Mshauri Elekezi (Consultant) Sky Architect Consultancy Ltd.
Eneo hilo ambalo VETA itajengwa lipo Kashai (MUVA) katika Manispaa ya Sumbawanga na lina ukubwa wa 95,934 sq M Plot 1 Block ‘A’ (LD) chenye hati Namba 44102-MBYLR iliyotolewa tarehe 5 Machi, 2018.
Mradi unategemewa kukamilika ndani ya miezi 12 (kuanzia tarehe ya makabidhiano). Aidha, gharama za ujenzi za mradi huu ni Tsh. 10,700,488,940.05. Ujenzi ukikamilika chuo kitaweza kuchukua wanafunzi 900 wa kozi ndefu na 600 wa kozi fupi hivyo, kitakuwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 1,500.
Regional Block, 90 Mwl. Julius Nyerere Road
Sanduku la barua: Box 128 Sumbawanga
Simu: 025 280 2137
Simu: 0756941328
barua pepe: ras@rukwa.go.tz
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa