Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Mkurugenzi wa manispaa ya Sumbawanga kuhakikisha wanaweka vibao vya kutambua barabara zilizopo katikati ya mji huo ili wananchi pamoja na wageni waweze kuzitambua.
Amesema kuwa mji wa Sumbawanga umependezeshwa na barabara hizo zilizojengwa na mradi wa uboreshaji miji kwa ufadhili wa benki ya dunia na hivyo si vyema barabara hizo zikawa hazitambuliki kwa majina yake huku akitolea mfano barabara ya Nyerere miongoni mwa barabara za mwanzo kujengwa wakati mji ukianza kukua na kuwa barabara hiyo haina utambuzi wa kibao chochote.
“Hapa Sumbawanga tunazo barabara na mitaa lakini hata hapa wajumbe tunaulizana hiyo Nyerere “road” iko wapi hatuna uelewa wa pamoja wengine wanajua wengine hawajui, barabara ya mahakama wengine wanajua wengine hawajui sasa mkurugenzi wa manispaa andaeni vibao ili vionyeshe huu ni mtaa gani na hii ni barabara gani, mji wetu umeanza kupendeza na kuwa na barabara nzuri na taa zake zinawaka lakini hakuna vibao vinavyoonyesha mtaa wala barabara,” Alisema.
Ameyasema hayo katika kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa kilichowashirikisha Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), Wakuu wa Wilaya, Wabunge, Wakurugenzi wa halmashauri pamoja na Wenyeviti wa halmashsuri za Mkoa huo.
Manispaa ya sumbawanga ni miongoni mwa halmashauri 18 zinzonufaika na program ya uimarishaji mijiunaosimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) na kufadhiliwa na benki ya dunia ambapo barabara mbalimbali zilizopo katikati ya mji zenye jumla ya urefu wa kilometa 11.577 zimejengwa kwa kiwango cha lami.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa