Serikali imetenga shilingi bilioni 4.5 kwaajili ya ujenzi wa hospitali tatu za wilaya za Mkoa wa Rukwa ili kuboresha huduma zinazotolewa na serikali kwa asilimia mia moja baada ya wilaya hizo kutokuwa na hospitali zake tangu kuanza kwa Mkoa huo mwaka 1974.
Wakati alipokuwa akiongea na wananchi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema kuwa mbali na ujenzi wa hospitali hizo za wilaya pia serikali imeendelea kutoa fedha kwaajili ya ujenzi wa hospitali mpya ya rufaa na kusisitiza kuwa hospitali ya sasa ya rufaa itatumiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kama hospitali yake ya Wilaya.
Hospitali hizo ambazo zinategemewa kujengwa katika Wilaya ya Nkasi, Kalambo pamoja na Sumbawanga Vijijini katika Kata ya Mtowisa iliyopo katika bonde la ziwa Rukwa zinategemewa kutoa msaada mkubwa kwa wananchi ambao wanaoishi mbali na makao makuu ya Mkoa na hatimae kuipinguzia mzigo hospitali ya rufaa ya Mkoa iliyopo sasa.
“tumedhamiria Seriakli lazima hizi hospitali tatu zijengwe, moja huku katika Halmashauri ya wilaya ya sumbawanga eneo la Mtowisa, Wilaya ya Kalambo na Wilaya ya Nkasi na kila Wilaya imetengewa Shilingi Bilioni 1.5 na wakati ukifika tutahamasishana kama tulivyofanya kwenye vituo vya afya ili tushambulie kama mchwa na ndani ya muda mfupi iwe tumemaliza,” Alisema.
Mkoa wa Rukwa una Hospitali moja tu ya Rufaa, vituo vya afya 12, na zahanati 172 amabazo zipo chini ya usimamizi wa asilimia mia moja wa serikali ya Tanzania, huku kukiwa na hospitali 2, vituo vya afya 8 na Zahanati 11 zinzomilikiwa na taasisi za kidini pamoja na zahanati 13 zinazomilikiwa na watu binafsi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa