Serikali imesema itajenga majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga ili kukihamisha kutoka kwenye majengo ya Kanisa Katoliki ambayo yamekuwa yakitumika kwa muda.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profess Joyce Ndalichako akiwa mkoani Rukwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa katika mikoa ya Rukwa na Katavi ambapo amesema kwa sasa ni vigumu kufanyia ukarabati majengo yanayotumika kwa sababu si maliya serikali.
Waziri Ndalichako amesema suala la uboreshaji wa miundombinu ya chuo hicho lipo ingawa changamoto iliyopo ya eneo pamoja na majengo kuwa si mali ya chuo hicho na kwamba kanisa Katoliki wanalihitaji eneo hilo kwa matumizi mengine.
“Chuo Cha Ualimu Sumbawanga hakijasahaulika katika kufanyiwa ukarabati, changamoto iliyopo ni kuwa eneo hili mlikaribishwa lakini mkang’ang’ania sasa wenyewe wanataka eneo lao ” alisisitiza Waziri Ndalichako.
Aidha Waziri amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19 kiasi cha shilingi bilioni 36 kimetengwa kwa ajili ya kuvifanyia ukarabati vyuo saba vya Ualimu, huku Chuo Cha Ualimu Murutunguru na Kabanga vikitarajia kujengwa upya.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo amesema anawashukuru Kanisa Katoliki jimbo la Sumbawanga kwa kuruhusu Chuo hicho kufanya shughuli zake katika eneo lake kwa muda mrefu, kwani mwanzoni kanisa hilo lilijenga majengo hayo ili kwa lengo la kuanzisha chuo cha kilimo.
Mkuu huyo wa mkoa amesema tayari mkoa wake umeshatafuta eneo lingine ambalo Chuo hicho kitahamishiwa, na kuwa hivi sasa tayari Mkoa umesharatibu taratibu za kuanza kulipa fidia kwa wakazi ambao eneo lao litachukuliwa kwa ajili ya matumizi ya Chuo hicho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa