Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatahadharisha wananchi wote watakaotumia mifuko ya plastiki kwa kuitumia kiuza, kusambaza, kubebea ama kuimiliki kwa namna yoyote ile kwani kwa kufanya hivyo watahatarisha uhuru wao na kuongeza kuwa kutokana na gharama kuongezeka ili kuipata mifuko mbadala amewataka wananchi kuanza kutumia mifuko ya kaki ama magazeti ya zamani kufungia sukari ama unga.
Amesema kuwa Mkoa umejipanga na wataalamu wake mbalimbali watendaji, kuanzia ngazi ya vitongovi, vijiji, mitaa, kata, halmashauri na wilaya zote kuhakikisha mifuko hiyo ya plastiki haitumiki na kubainisha kuwa kwasababu kanuni zipo na zimefafanua vizuri hivyo hakuna sababu za kutafuta visingizio ili kuweza kukwepa adahabu kwa atakayekiuka sheria hiyo.
“Tutaendelea kuona ni changamoto gani ambazo zinatukabili sisi, najua kama nilivyosema mifuko mbadala huenda isiwe mingi sana lakini hii haizuii watu kufanya shughuli zao kubebea, kuna vitu vingi, kuna vikapu, mbona zamani tulikuwa tunatumia mifuko ile ambayo ni ya kaki, unatengeneza unaweka gundi, lakini ukienda kwenye duka unakuta zile karatasi za magazeti wanakukunjia wanakuwekea sukari yako mule unaondoka, tutarudi huko,” Alisisitiza
Na kuongeza kuwa kadiri siku zinavyozidi kusogea mifuko mbadala itajaa na pia alitumia fursa hiyo kuwaasa wajasiliamali kuitumia fursa kuweka viwanda vidogovidogo vya kuzalisha mifuko mbadala.
Katazo hilo limetokana na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (Environmental Management Act) serikali ya Tanzania imetunga kanuni za mwaka 2019 za kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.
Kifungu cha nane cha kanuni hizo kinaorodhesha makosa matano ambayo ni; kuzalisha na kuagiza mifuko ya plastiki, kusafirisha nje ya nchi mifuko ya plastiki, kuhifadhi na kusambaza mifuko ya plastiki, kuuza mifuko ya plastiki na mwisho kumiliki na kutumia mifuko ya plastiki.
Kila kosa lina adhabu yake kwa mujibu wa kanuni hizo kulingana na uzito wa kosa lenyewe.
Kwa kosa la kwanza la uzalishaji na uagizaji adhabu yake ni mosi,faini isiyopungua TSh milioni 5 na isiyozidi TSh milioni 20, pili kifungo kisichozidi miaka miwili jela, adhabu ya tatu ni mjumuiko wa adhabu zote mbili za awali faini na kifungo.
Adhabu za kosa la pili amabalo ni kusafirisha mifuko nje ya Tanzania ni sawa na za kosa la kwanza.
Kwa kosa la tatu la kuhifadhi na kusambaza mifuko adhabu zake ni mosi faini isiyopungua TSh milioni 5 na isiyozidi TSh miioni 52, pili kifungo kisichozidi miaka miwili, tatu faini na kifungo kwa pamoja.
Ukipatikana na hatia ya kuuza mifuko ya plastiki adhabu ambazo utakumbana nazo ni mosi, faini isiyopungua TSh laki moja na isiyozidi laki tano, pili, kifungo kisichozidi miezi mitatu jela na tatu yawezekana ukahukumiwa adhabu zote mbili za awali kifungo na faini.
Ukiendelea kutumia na kumiliki mifuko ya plastiki kuanzia Juni 1 nchini Tanzania, basi jiandae kulipa faini isiyopungua TSh30,000 na isiyozidi laki mbili, kifungo kisichozidi siku saba ama faini na kifungo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa