Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameitahadharisha bodi ya shule ya Sekondari Kantalamba kuhakikisha wanaweka mikakati ya kuondoa daraja la sifuri katika shule hiyo kongwe nchini iliyoanzishwa mwaka 1964 na Kanisa Katoliki na hatimae kukabidhiwa rasmi serikali mwaka 1968.
Amesema kuwa shule hiyo haina hadhi ya kuwa na daraja la sifuri kutokana na kutoa viongozi mbalimbali walioiongoza nchi hii na kuwa serikali kwa makusudi imetoa shilingi Bilioni 1.1 ili kuboresha miundombinu ya shule hiyo hivyo haipendezi kusikika ikiendelea kutoa daraja la sifuri kuanzia kidato cha pili hadi cha sita.
“Mjumbe wa bodi ziondoeni hizi sifuri zitoke kabisa, na hata four taratibu zitoeni, yaani hapa pana hadhi ya Division one nyingi, two zinafuata na three mwisho hiyo ndio hadhi ya Kantalamba sekondari na ukongwe wake, na sasa tunatumia mabilioni kuboresha miundombinu halafu bado sifuri, sifuri katika mazingira haya, na anakaa bweni miaka minne sifuri?” Alisema.
Ameyasema hayo alipotembelea shule hiyo ili kujionea marekebisho ya ujenzi wa majengo kadhaa yaliyofanywa ili kuboresha mazingira ya shule kwaajili ya wanafunzi.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule Hiyo Martin Kasensa amesema kuwa ufaulu wa wanafunzi umekuwa ukipanda mwaka hadi mwaka.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa