JAMII YAASWA KUJENGA UTAMADUNI WA KUWAHUDUMIA WAZEE
Jamii imeaswa kujenga utamaduni wa kuwaheshimu na kuwahudumia wazee badala ya kutegemea tu sheria zilizopo, kwani bila mtazamo chanya wa kijamii, juhudi za serikali hazitakuwa na mafanikio ya kudumu.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Ndg. Hajjayand Adon, wakati akifungua kikao cha Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa wa Rukwa, kilichofanyika tarehe 19 Machi 2025, katika Ukumbi Mdogo wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa amesema kuwa mahitaji ya wazee wengi ni ya msingi na yanaweza kutatuliwa na jamii endapo utamaduni wa kuwahudumia wazee utajengwa kwa dhati. Amesisitiza kuwa wazee wengi ni wale waliotulea na kutufikisha hapa tulipo, na kwa umri wao, mahitaji yao makubwa ni chakula, malazi na matibabu, ambayo gharama yake si kubwa kwa jamii.
Ameeleza kuwa bila jamii kubadili mtazamo na kuendeleza utamaduni wa kuwaheshimu na kuwahudumia wazee, sheria pekee hazitakuwa na tija katika kuhakikisha ustawi wa wazee.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa wa Rukwa, Ndg. Timoth Makaza, amesema kuwa licha ya uwepo wa sera na sheria za kusaidia wazee, bado kuna haja ya kuziboresha na kuhakikisha utekelezaji wake unawanufaisha wazee kwa uhalisia.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Rukwa, Ndg. Godfrey Mapunda, amesema kuwa hadi sasa mkoa umefanikiwa kutoa vitambulisho vya matibabu bila malipo kwa wazee 19,994, sawa na asilimia 58 ya wazee waliotambuliwa. Hatua hii ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha wazee wanapata huduma za afya kwa urahisi na bila gharama.
Serikali na wadau wa maendeleo wamehamasishwa kuendelea kuwekeza katika sera bora na mipango madhubuti itakayohakikisha maisha bora kwa wazee, huku jamii ikihimizwa kushiriki kikamilifu katika kuwatunza na kuwaheshimu wazee kwa vitendo
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa