Wananchi wa Halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa wamemuomba mkuu wa Mkoa huo kamishna Mstaafu Zelote Stephen Kufanya maonyesho ya Nane nane Kimkoa ili wakulima na wafugaji wasioweza kufika katika ngazi ya kanda wapate fursa ya kuelimika na kuonesha bidhaa zao Kimkoa.
Maombi hayo yametolewa na wananchi wa Manispaa hiyo baada ya Mh. Zelote Stephen kutembelea mabanda kadhaa ya maonesho ya nanenane yaliyofanyika katika Manispaa hiyo kwenye kituo cha kilimo katika Kijiji cha Katumba azimio ili kutoa fursa kwa wakulima na wafugaji wadogo kuonyesha bidhaa zao.
“mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wanaokwenda kwenye maonyeshoi ya nanenane kanda ni wachache sana na wengi tuliopo hatuna vipato vya kutosha kutufikisha huko, hivyo tunaomba tufanye nane nane ya Kimkoa ili nasi tuweze kuonyesha bidhaa zetu na tuweze kujifunza kwa wenzetu,” Alisema Pscal Mwanisawa Mkulima wa Kijiji cha Ulinji Manispaa ya Sumbawanga.
Kuwepo kwa maonyesho hayo ni utekelezaji wa pendekezo la Mh. Zelote aliyetaka kila halmashauri kufanya maonesho ili wakulima na wafugaji waweze kuelimishana na kutambulika katika maeneo yao ili wapate msaada kutoka kwa maafisa ugani ili kuongeza tija katika kilimo na ufugaji na hatimae kuongeza thamani katika mazao yao.
Akipokea maombi hayo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amesema kuwa ili wananchi waweze kujikwamua ni muhimu kuungana na kuwa na utambulisho wa aina moja wenye bidhaa tofauti katika makundi yao ili kuwa na nguvu.
“Muitikio wa wakulima na wafugaji katika Mkoa wa Rukwa upo juu sana, ila hawapewei nafasi, sasa mwakani ni lazima kwa Halmashauri zote kufanya nane nane katika Halmashauri zao. Nitasimamia kila mtu apate nafasi ili kujifunza teknolojia mpya na tuachane na mambo ya zamani,” Mh. Zelote alisema.
Katika kuunga mkono ombi la wananchi hao Mbunge wa Viti maalum Mh. Silafi Maufi, alipongeza juhudi za Mh. Zelote kwa kuhakikisha wananchi wa Halmashauri wanapata nafasi ya kuonesha bidhaa zao mbali na kuongeza kuwa ni jambo linalowezekana kufanya “Nane nane” ya kimkoa.
“ mheshimiwa mkuu wa Mkoa umekuwa shahidi kwa namna maonyesho yalivyofana ni Dhahiri kuwa inawezekana kufanya nane nane ya kimkoa katika mkoa wetu wa Rukwa,” Mh. Maufi alimalizia.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa