IMEBAINIKA kuwa mabaraza ya ardhi ngazi ya vijiji na kata yamekua ni chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi na kuwa ipo haja kwa serikali kutizama upya mfumo huo wa mabaraza.
Hayo yamesemwa na katibu tawala wa wilaya Nkasi Cosmas Kuyela kwa niaba ya mkuu wa wilaya Nkasi Said Mtanda kwenye uzinduzi wa wiki la sheria Nchini ambapo amesema kuwa lengo la serikali la kuweka masbaraza ni zuri lakini sasa imekuwa ni tofauti kwa wao kuwa chanzo chas migogoro mikubwa.
Alisema kuwa kupitia wiki hili la sheria Nchini ni muhimu kwa serikali kuuangalia upya mfumo huo wa mabaraza ya ardhi ya kata na ikiwezekana iangalie namna nyingine ya nabaraza kama hayo ambayo yatakua na tija kwa jamii kuliko kama ilivyo sasa.
‘’mabaraza haya ya kata na vijiji yanatupa shida sana sisi viongozi wa wilaya kwani kero imekuwa kubwa sana kwa Wananchi na ukiangalia asilimia kubwa ya kero zinazofika ofisini kwetu ni migogoro ya ardhi ambayo mingi imetokana na mabaraza ya ardhi sasa badala ya mabaraza haya kuwa mkombozi lakini sasa ndiyo yamegeuka kuwa tatizo’’alisema
Pia amebainisha kuwa matumizi ya lugha ya Kiingereza katika Mahakama ni chanzo cha wengi kukosa haki hivyo ipo haja kwa mahakama kuliona hilo ili mashauri na majalada yote ya kimahakama yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili ambacho Watanzania wengi wanakifahamu
Alidai kuwa Wananchi ambao ndiyo walengwa wa huduma hizo za kimahakama wengi wao hawajui kabisa kiingereza na kuwa kitendo cha mahakama kutumia kiingereza katika nyaraka zao kinawaongezea gharama wananchi ya kwenda kwa Watu ili kuweza kupata tafsiri ya kile kilichoandikwa
Na aliitataka jamii kuitumia fursa hiyo ya wiki ya sheria nchini kwa kwenda kupata elimu kwa Wanasheria kitu kitakachowapelekea wao kuwa walau na uelewa wa masuala ya kisheria
Hakimu mkazi mfawidhi wa makama ya wilaya Benedict Nkomola kwa upande wake aliwataka wananchi wote kwa ujumla kujitokeza katika wiki hili la sheria katika viwanja vya mahakama ambapo watapata elimu na kuielewa vyema idara hiyo ya mahakama inavyofanya kazi
Alisema kuwa wiki la sheria ni mwanzo wa kuanza kwa shughuli za kimahakama hapa nchini kwa mwaka huu wa 2021
Maadhimisho ya wiki la sheria mwaka huu yamebeba ujumbe usemao “miaka 100 ya mahakama kuu ;mchango wa Mahakama katika kujenga nchi inayozingatia uhuru ,haki,ududu,amani na ustawi wa wananchi 1921-2021’’
mwisho
Na Israel Mwaisaka,Nkasi
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa