Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, amewataka wazazi na walezi kuzingatia lishe kwa watoto katika siku 1000 za kwanza za ukuaji ili kujenga jamii yenye afya bora.
Mheshimiwa Makongoro ameyasema hayo leo Julai 09, 2024 alipokuwa akikabidhi vitabu vya kliniki kwa Waganga Wakuu wa Wilaya za Sumbawanga, Nkasi, Kalambo, na Manispaa ya Sumbawanga. Zoezi la ugawaji wa vitabu hivyo limefanyika katika Kituo cha Afya Mazwi kilichoko Manispaa ya Sumbawanga.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amewataka waganga wakuu wa Halmashauri zote Mkoani Rukwa kufikisha vitabu na kuhahikisha vinatumika kama ilivyokusudiwa huku akisisitiza kuwa vitabu hivyo vinatolewa bure kwa walengwa. Amesema lengo la Serikali kutoa vitabu hivyo ni kufanya ufuatiliaji wa karibu afya ya mama na mtoto.
Jumla ya vitabu 34,954 vimekabidhiwa kwa waganga wakuu wa Halmashauri zote za Mkoa wa Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa