Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo amewashauri Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoani Rukwa kukutana na madiwani pamoja na wenyeviti wa halmashauri zinazopitiwa na barabara ya Tunduma – Sumbawanga ili kuyabaini matuta yaliyowekwa maeneo ambayo hayana ulazima hivyo kutostahili kuendelea kuwepo kwenye barabara hiyo na hatimae kujiandaa kuyapunguza wakati wakiendelea kusubiri maamuzi ya Wizara.
Amesema kuwa endapo zoezi hilo litakuwa shirikishi halitazua mzozo baina ya TANROADS na wananchi pindi ajali zitakapoongezeka na kuwataka wabunge wa maeneo husika nao kukubaliana na maamuzi yatakayotolewa na wizara husika baada ya utambuzi huo wa matuta kufanyika.
“Kuna ukweli kwamba kuna baadhi ya Matuta hayastahili kuendelea kuwepo, matuta zaidi ya 200 lakini kuna baadhi yao yapo maeneo ambayo hayastahili kuwepo, mi nadhani kungefanyika utambuzi wa matuta ambayo sio ya lazima, halafu ndio hoja inakuwa kwamba kuna matuta Fulani ambayo sio ya lazima yapo katika maeneo Fulani ambayo hata waheshimiwa madiwani wa maeneo yale wameyaafiki kwasababu hii isiwe kazi ya TANROADS peke yao,”Alishauri.
Ameshauri hayo katika kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa kilichowashirikisha Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), Wakuu wa Wilaya, Wabunge, Wakurugenzi wa halmashauri pamoja na Wenyeviti wa halmashsuri za Mkoa huo.
Ushauri huo umekuja baada ya mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini Mh. Aeshi Hilary kuilalamikia TANROADS kuhusu wingi wa matuta hayo na matokeo yake kuwakera wasafiri wanaotumia barabara hiyo jambo ambalo limekuwa likiwachosha wasafiri wanaotoka mikoa ya mbali na Mkoa wa Rukwa.
“Utakuta kuna matuta ambayo yanawekwa sehemu ambapo wala hayastahili, barabra hii ya Tunduma – Sumbawanga ina matuta zaidi ya 240 inazidi hata kilometa za barabara yenyewe, kuna tuta lipo katikati ya daraja, kwa mfano kuna Kijiji cha Tamasenga peke yake kina matuta kumi, kuna umuhimu gani wa kuyaweka yote hayo katika Kijiji kimoja, mlisema mtayaondoa lakini hapa kwenye bajeti yenu sioni kama mmelizungumzia,” Aliuliza.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoani Rukwa Mhandisi Masuka Mkina alibainisha kuwa uwepo wa matuta hayo umepunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani na kuongeza kuwa wafadhili waliowezesha ujenzi wa barabara hiyo kauli mbiu yao ilikuwa ni “Usalama Kwanza”.
“Alipokuja hapa Katibu Mkuu Nyamhanga nilizungumza lakini baadae akasema tuyaache kwanza, kwahiyo suala la matuta kwa sasa mimi sina la kuzungumza kwasababu serikali bado wanaendelea kulitafakari kwamba wayatoe au yabaki, kwasababu yamesaidia sana ukiangalia takwimu kwa barabara ya Tunduma - Sumbawanga ajali nikama sifuri,” Alisema.
Barabara ya Tunduma – Sumbawanga yenye kilometa 227 inakadiriwa kuwa na matuta 212 huku madatuta kadhaa yakiwa katikati ya madaraja na Kijiji cha Tamasenga kuwa na matuta 10 imefadhiliwa kwa msaada wa watu wa Marekani imesaidia kurahisisha safari ya Tunduma kwenda Sumbawanga ambapo hapo kabla wasafiri walitumia siku nzima.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa