Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Omary Mgumba amewahakikishai wakulima wa zao la mahindi mkoani Rukwa kuwa mradi wa ujenzi wa Vihenge vya kisasa vya kuhifadhia mazao hayo utakapokamilika utatatua tatizo la soko kwa wakulima ambao kwa msimu wa 2019/2020 wamekuwa wakipata tabu kutokana na wanunuzi wengi kutoka nchi za jirani kufunga mipaka yao kutokana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19) na hivyo kushindwa kuingia nchini kwetu na kununua mazao hayo.
Mh. Mgumba amesema kuwa hivi sasa NFRA wamesiama kununua mazao kwasababu ya kufanya tathmini kwa wakulima wanaoidai fedha NFRA ambapo hadi kufikia tarehe 18.9.2020 hakukuwa na mkulima hata mmoja anayedai fedha hizo na kuongeza kuwa kutokana na maghala mengi ya NFRA kujaa imewapelekea kushindwa kununua mengine huku akitanabahisha kuwa serikali haitaki kuwakopa wakulima wakitambua kuwa wakulima hao hivi sasa wanajiandaa na msimu mpya wa kilimo.
“Lakini la pili ambalo walisimama na sehemu nyingine wakaendelea kusimama, ni kutokana na maghala yamejaa, pa kuweka hakuna, Ushahidi ni nyinyi watu wa Laela, ndio maana nikataka kuhakikisha kwa kuingia ndani kwanza, nimekuta humo ndani kumejaa, pa kuweka hakuna na ndio maana kama serikali tuliwawezesha NFRA kujenga maghala mapya na vihenge vipya ili kuongeza uwezo wa NFRA kuhifadhi mahindi mengi Zaidi na kununua mahindi mengi Zaidi kutoka kwa wakulima na watu wengine,” Alisema.
“Kuyumba kwa soko ni sababu ya janga la ugonjwa wa Corona, ndio maana mnaona wanunuzi kutoka nchi jirani zinazotuzunguka, Rwanda, Kenya, Uganda, Congo wamepungua sana mwaka huu na kama wakija ni wachache sana, kwasababu huko kwao bado wamejifungia kutokana na athari ya ugonjwa wa Corona, kwahiyo wanunuzi tumebaki sisi wenyewe Watanzania, mtu achukue hapa apelike labda Dar, Dodoma, Morogoro ama Mwanza, kwa bahati nzuri mwaka jana tumepatya neema ya mvua imenyesha vizuri kwahiyo sehemu kubwa mpunga umekubali, na mahindi yamekubali kwahiyo tunatarajia hii hali itakuwa ya muda baada ya janga la Corona kupungua huko nchi za jirani masoko yatafunguka na hali itakuwa nzuri,” Alisisitiza.
Wakati akitoa taarifa ya Ununuzi wa mahindi pamoja na uhifadhi wake katika mikoa ya Rukwa na Katavi, Kaimu Meneja wa kanda ya Sumbawanga inayojumuisha mikoa hiyo Marwa Range alisema kuwa kwa sasa NFRA wanaweza kuhifadhi mazao kwa jumla ya tani 38,500 na mradi wa maghala na vihenge utakapokamilika uwezo wa kuhifadhi mazao utaongezeka hadi kufikia tani 58,500 kwa mkoa wa Rukwa pekee, huku Mkoa wa Katavi ukiwa na uwezo wa kuhifadhi tani 500 kwa sasa lakini mradi huo ukikamilika mkoa utaweza kuhifadhi tani 28,000 na kuifanya NFRA kanda ya Sumbawanga kuwa na uwezo wa kuhifadhi jumla ya tani 86,500 za mazao.
“Kwa msimu huu wa 2020/2021 kanda ya Sumbawanga ilipangiwa kununua tani 55,000 za mahindi katika vituo vyake vikuu na vidogo kutokana na changamoto za maghala baadhi ya vituo havikuweza kufunguliwa kwa kukosa maghala maeneo ya kununulia mahindi, mfano kwa mkoa wa Katavi kituo cha mpanda kutokana na shughuli za ujenzi wa vihenge zinazoendelea na maghala ya watu binafsi kuchukuliwa na vyama vya ushirika tumeshindwa kufungua kituo hiki kwa kukosa sehemu ya uhifadhi,” Alisema.
Kwa upande wake Mhandisi mkaazi wa Mradi wa ujenzi wa Vihenge kutoka Wakala wa Majengo (TBA) Mkoani Rukwa Mhandisi Haruna Kalunga amesema kuwa mradi huo unaotarajiwa kukamilika tarehe 3.3.2021 utafikia asilimia 60 mwishoni mwa mwezi Septemba na kubakisha asilimia 40 inayotarajiwa kumaliza ndani ya miezi iliyobakia.
“Tuna Vihenge nane, sita vikubwa, vidogo viwili, vitano vimeshakamilika kimoja kinaendelea na ujenzi, viwili bado havijakamilika lakini misingi ya vihenge imeshakamilika na ghala la nje ambalo nalo limefikia kwenye hatua ya kupandisha jengo juu kwa maana ya kujenga kolamu, ujenzi wake unaendelea na huduma saidizi kwa maana ya ‘Dryer’ tayari imeshakamilika, sehemu ya kupokelea mazao imeshakalimika, Burner na vifaa vyote, vimeshawasili,” Alieleza.
Katika hatua nyingine Mh. Mgumba aliwasifu wakandarasi wa ujenzi wa vihenge hivyo vya kisasa kwa kuwa ndani ya wakati Pamoja na shughuli zao hizo kuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo janga la Corona lakini wameweza kufanikisha kuifanya kazi hiyo kwa wakati na kuwatumia wafanyakazi watanzania kwa asilimi kubwa na hivyo kuinufaisha nchi kwa kuzalisha wataalamu wa ujenzi wa vihenge hivyo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa