Mwananchi wa Kijiji cha Mtowisa, Kata ya Mtowisa, Tarafa ya Mtowisa, Wilayani Sumbawanga Pius Wapinda ameshangazwa na kitendo cha taasisi mbalimbali za kiserikali kuweka visanduku kwaajili ya kukusanyia maoni ya wananchi lakini hakuwahi kupata mrejesho wa maoni hayo kufanyiwa kazi.
Mwananchi huyo aliiomba serikali kuyafanyia kazi maoni hayo na kufanya mrejesho kupitia mikutano na vikao mbalimbali vinavyofanywa na serikali katika ngazi tofauti ili wananchi wawe na moyo wa kuendelea kutoa maoni hayo pindi wanapoona yanafanyiwa kazi.
“ukipita kwenye maofisi ya kiserikali kuna masunduku mbalimbali pale, yale masanduku ya maoni mimi huwa sioni kama yana maana yoyote na sijui yanatusaidia kitu gani maana sioni mrejesho wake, ningependelea kwenye mikutano kama hii wangekuwa wanatuambia kuanzia mwezi wa kwanza hadi wa kumi tumepokea maoni kadhaa na mrejesho wake ni huu hapa,” Alieleza.
Nae Afisa utumishi wa Halamashuri ya Wilaya ya Sumbawanga Hamis Mangale alisema kuwa ni mwezi mmoja tu tangu akabidhiwe ofisi hiyo na hakufahamu kama utaratibu wa dawati la malalamiko halifanyiwi kazi hivyo aliahidi mbele ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo kulichukua hilo na kuhakikisha wanalifanyia kazi ili kukata kiu ya wananchi ambao wengi wamekuwa na malalamiko yanayohusu masuala ya mapenzi.
Katika Kusisitiza hilo Mh. Wangabo alisema kuwa maoni hayo ni vyema yakachukuliwa na taasisi husika ikiwa ni hospitali kuna kamati ya afya, yajadiliwe katika kamati hiyo na hatimae wananchi wapatiwe mrejesho katika vikao mbalimbali kuanzia ngazi ya Kijiji hadi kata.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa