Na Israel Mwaisaka,Rukwa
NAIBU Waziri wa afya na ustawi wa jamii Mh. Dkt.Godwin Mollel amekiri kuwepo kwa changamoto juu ya mfumo wa Bima ya Mfuko wa Afya ya Jamii na kuwa wizara imeliona na inakwenda kulifanyia kazi.
Hilo amelisema jana alipokuwa akizungumza na Watumishi wa idara ya afya wa wilaya ya Nkasi kwenye jengo jipya la hospitali ya wilaya baada ya kupata malalamiko kutoka kwa mbunge wa jimbo la Nkasi Kasikazini Mh. Aida Khenan ambaye alisema kuwa huduma za afya kupitia bima hiyo hazina uhalisia wa kile kinachotarajiwa.
Dkt. Mollel alisema kuwa kinachoangaliwa ni mfumo wa bima ambapo kwa sasa fedha zinaenda ofisi ya mkuu wa mkoa na kisha kuna asilimia zinazokwenda vituo vya afya kupitia wilayani na kuwa hilo wameliona na watakwenda kutafuta ufumbuzi ili kasoro zitakazobainika ziondolewe.
Pia Dkt. Mollel aliitumia fursa hiyo kuwafunda watumishi wa afya kufanya kazi zao kwa weledi na kuwa wao kama wizara wamebaini mambo mengi ya hovyo yanayofanywa na watumishi hao na kuwa sasa wanachokifanya ni kukutana nao na kuelezana ili baadae watakapoanza kuchukua hatua kusiwepo na lawama.
Alisema kuwa changamoto ya dawa inayopatikana katika hospitali zetu ni matokeo ya utendaji hafifu kwa baadhi ya watendaji katika idara kwa kuwa serikali ilishatoa muongozo mzuri wa upatikanaji wa dawa na kuwa ukosefu wa dawa katika baadhi ya hospitali ni wizi na kutowajibika kwa watendaji hao.
‘’sisi kama wizara tumebaini madudu mengi yanayofanywa katika hospitali zetu na ndiyo maana tumekubaliana tupite kwanza kwa watumishi tuwafunde ili ukifika wakati tusilaumiane kutokana na maamuzi hayo magumu’’alisema
Awali mkuu wa wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda alimweleza Naibu Waziri huyo kuwa ujenzi wa hospitali ya wilaya umekamilika kwa asilimia 97 huku Tshs,Bil.1.8 zimeshatumika kwenye ujenzi wa hospitali hiyo.
Alisema kuwa kilichobaki sasa ni kuiomba serikali iwapelekee mahitaji muhimu yanayotakiwa ili hospitali hiyo ifunguliwe rasmi na watu kuendelea kupata huduma za kiafya.
Ndipo naibu waziri alipomtaka mganga mkuu wa wilaya kuandika mahitaji muhimu yanayotakiwa kwenda MSD haraka ili hospitali hiyo iendelee kufanya kazi.
Mwisho
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa