Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amekataa maombi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kufanya ukandarasi wa majengo mbalimbali ya serikali mkoani Rukwa kutokana na kusimama kwa mradi wanaousimamia kutokamilika kwa muda wa miaka minne.
Maombi hayo yaliwasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa na meneja wa Mkoa wa shirika hilo Mhandisi Musa Kamendu baada ya Mh. Wangabo kutembelea mradi wa nyumba 20 za NHC zilizopo sumbawanga mjini ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa nyumba hizo ambazo umefikia asilimia 60.
Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 ambao ulianza mwezi juni 2014 na kusimama kutokana na shirika kukosa fedha za kuendeleza na kutarajiwa kuendelea ifikapo mwezi machi mwaka huu amabpo hadi kufikia hapo shilingi 867,990,367 zimeshatumika kati ya 1,532,473,872.
“Tunaona wakati mwwingine serikali inatoa kazi kwa SUMA JKT na kukarabati shule kama Kantalamba Sekondari, sisi kama mkandarasi daraja la kwanza, Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine tunawaalika na tunawaomba mtupe hizo kazi, tutazifanya vizuri sana na kwa ufanisi mkubwa, tumesikia kuna miradi mingi, sisi kama wakandarasi tunaomba mtupe hizo kazi,” Mhandisi Kamendu alimalizia.
Katika kujibu maombi hayo Mh. Wangabo alitoa angalizo kuwa endapo mradi wa shirika umeshindikana kumalizika kwa wakati hali hiyo itakuwaje kama wakipewa mradi na taasisi nyingine ya serikali na kuwataka kwanza kumaliza mradi wao ili wawe na ushahidi wa kuonekana katika Mkoa wa Rukwa na sio kuishia kutoa mifano kwa miradi iliyofanyika katika mikoa mingine.
Thamani ya nyumba moja ni shilingi 139,680,000 na ikiwa haikumalizwa gharama yake ni shilingi 118,080,000 bila ya VAT.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa