Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere ameagiza kufanyika kwa uchunguzi kuhusu ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Mheshimiwa Makongoro ameagiza uchunguzi huo Juni 24, 2024 alipohudhuria kikao cha Baraza maalum la Madiwani lililoketi kupitia na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kuishia Juni 2023.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ametoa maagizo hayo kufuatia mwenendo usioridhisha wa ukusanyaji wa mapato Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ambao umekuwa ukishuka kila Mwaka kwa miaka mitatu mfululizo. Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuishia Juni 2023 inaonesha kuwa kiwango cha makusanyo kimekuwa kikipungua kutoka asilimia 89 kwa Mwaka 2021/2022 hadi asilimia 75 kwa Mwaka 2023/2024.
Mheshimiwa Makongoro ametaka uchunguzi uhusishe namna vyanzo vya mapato vinavyoibuliwa, takwimu za vyanzo vya mapato vilivyopo (revenue collection data base), namna ukusanyaji unavyofanyika, malipo ya wakusanyaji ikiwa fedha zote zinawasilishwa benki kwa wakati kulingana na taratibu za fedha zinavyoelekeza.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ameitaka Halmashauri kuhakikisha Sheria,Taratibu na Kanuni za Fedha na Manunuzi zinafuatwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha udhibiti wa ndani.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa