Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewashukuru wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa kwa kuonesha ushirikiano usio kifani kuhakikisha mbio za Mwenge wa Uhuru zinafanikiwa.
Aliyasema hayo wakati wa Kuuaga Mwenge wa Uhuru na kuukabidhi Mwenge huo kwa Mkoa wa Songwe, Tukio ambalo lililofanyika katika Kijiji cha Mkutano kinachopakana na Mkoa wa Rukwa.
“Napenda nichukue nafasi hii kuwashukuru wote katika Mkoa wa Rukwa walioshiriki kwa namna yoyote ile kuhakikisha kwamba Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2017 zinafanikiwa na kwa kweli zimefanikiwa,” Mh. Zelote Stephen alisema.
Katika Kuelezea faida za kihisia za Mwenge wa Uhuru Mh. Zelote Stephen alisisitiza, “Tutaendelea kuenzi Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa ambao unaleta matumaini pasipo na matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipo na dharau.”
Pamoja na hayo hakusita kutoa wito kwa wananchi wa Rukwa juu ya kazi kubwa iliyofanywa na Mwenge wa Uhuru na hasa kuitekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya mwaka huu ya isemayo “Shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu.”
“Wito wangu kwa wananchi wote wa Rukwa kazi kubwa ambayo Mwenge wa Uhuru 2017 umeifanya katika Mkoa wetu ni mtaji ambao tunapaswa kuutumia kuleta maendeleo ndani ya Mkoa na hasa la viwanda jambo ambalo linawezekana kwa kuwa ni Mkoa wa uzalishaji mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi,” Mh. Zelote Stephen alimalizia.
Katik tukio hilo Mh. Zelote Stephen hakuacha kumshukuru Kiongozi wa wakimbiza Mwenge Kitaifa Amour Hamad Amour pamoja na wasaidizi wake, Salome Obadia Mwakitalima, Shukran Islam Msuri, Bahati Mwanigusha Lugodisha, Vatima Yunus Hassan pamoja na Fredrick Joseph Ndahani kwa ushujaa, uelewa na ukakamavu wao waliouonyesha ipindi chote walichokuwa katika Mkoa wa Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa