Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewataka wananchi kuwa na viambatanisho vya muhimu vitakavyowatambulisha kwa urahisi katika zoezi la uandikishwaji wa vitambulisho vya uraia.
Mh. Zelote ametoa rai hiyo alipokuwa akizindua na kukabidhi vitambulisho kwa baadhi ya watumishi wa Mkoa, Wilaya pamoja na Halmashauri.
“Andaeni viambatanisho muhimu vitakavyowasaidia kutambulika kwa urahisi.Viambatanisho vya msingi ni pamoja na vile vinavyohitajika kuthibitisha umri, Makazi na Uraia, kama vile cheti cha kuzaliwa, hati ya kusafiria, Vyeti vya shule, kadi ya kupigia kura, kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, TIN namba n.k. Kuwa na vitambulisho vingi ni kutambulika kwa haraka na kurahisisha uandikishaji,” Mh. Zelote alifafanua.
Zoezi hili la vitambulisho vya taifa lilianza kwa watumishi wa umma tarehe 3, October hadi 31, Disemba mwaka 2016, na kutegemewa kuanza uandikishwaji huo mnamo mwezi wa 6 mwaka huu kwa wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa.
Mkuu wa Mkoa pia hakusita kutoa ushauri kwa watendaji wa Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri ili kuwawezesha kila mwananchi kujiandikisha bila ya usumbufu.
Pamoja na hayo Mh. Zelote aliwatahadharisha kuwa katika uandikishwaji huo watakutana na watu aina tofauti hivyo ni jukumu lao kupanga namna ya kurahisisha huduma hiyo.
“Mkumbuke mtakutana na watu wa aina tofauti wakiwepo wazee, vijana, walemavu na waja wazito. Ni jukumu lenu kujipanga namna ya kurahisisha huduma kwao. Toeni ratiba zenu mapema kuwandaa wananchi. Shirikianeni na Watendaji wa Halmashauri ngazi ya Vijiji, Kata n.k.” Mh Zelote alieleza.
Katika kusisitiza suala la ushirikiano Mh. Zelote aliwaomba viongozi wa dini na siasa kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati na kujitokeza katika zoezi hili.
Miongoni mwa faida za vitambulisho hivi ni pamoja na kusaidia kuongeza wigo wa mapato ya serikali, kurahisisha kuhesabu watu, vitawezesha kumtambua mtu anapofanya biashara au shughuli nyingine kwa kutumia majina tofauti n.k.
Nae Afisa NIDA Mkoa wa Rukwa Emmanuel Mujuni aliwaomba wananchi kuwa na subira hadi hapo utaratibu utakapokamilika na kuweza kuwatangazia na hatimae zoezi hilo kuanza mara moja.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa