Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstafu Zelote Stephen Zelote amewatoa wasiwasi wakulima wanaolalamikia ubovu wa barabara vijijini kwa kusisitiza mpango wa serikali kuanzisha wakala wa barabara mijini na vijijini ili kuondoa kero hiyo.
Ameyasema hayo wakati alipokuwa akijibu hoja ya mmoja wa wakulima Frank Enock aliyeilalamikia serikali kushindwa kuboresha miundombinu vijijini ili kupata urahisi wa kusafirisha mazao kwa kipindi chote cha mwaka.
Hoja hiyo iliibuka wakati wa majadiliano katika mkutano wa uzinduzi mpango wa Taasisi ya Kuendeleza Mifumo ya Kimasoko katika Kilimo (AMDT) kwa alizeti uliofanyika Mkoani Songwe na kuhudhuriwa na wakuu wa mikoa mitatu ya Songwe, Rukwa na Katavi ambapo mgeni rasmi wa uzinduzi huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa.
Mbali na wakuu wa Mikoa mkutano huo pia ulijumuisha wakurugenzi wa Halmashauri, mafisa kilimo wa mikoa na halmashauri, wakulima, pamoja na wasindikaji wa mafuta ya alizeti huku lengo kuu likiwa ni kuboresha na kuwakomboa wakulima wadogo wa zao hilo
“Kuhusu suala la miundiombinu serikali imeliona hilo tatizo na ndio maana kimeanzishwa kitu kinaitwa TARURA wakala wa barabara mijini na vijijini kwaajili ya kuboresha barabara na kuona kuwa zinatengenezwa na zinapitika, kwahiyo msiwe na wasiwasi, barabara hizo zimelenga kuwainua wakulima kwa kuwawezesha kusafirisha mazao yao kwa urahisi na hatimae bei za vyakula kupungua kutokana na kurahisishwa kwa njia za kusafirishia,” Mh. Zelote alisisitiza.
Na kuongeza kuwa uanzishwaji wa wakala huo utaondoa ubabaishaji uliokuwa katika halmashauri ambazo hudanganya katika utekelezaji wao katika kujenga barabara za uhakika na ama kuzichelewesha.
Katika kukazia suala la maendeleo na nia ya serikali ya awamu ya tano katika kumkomboa mwananchi, Mh. Zelote alisisitiza msimamo wa Rais Dk. John Pombe Magufuli wa kuwainua wananchi wa kipato cha chini na kuwanaoangaliwa kwa jicho la pekee.
“Tukitaka kuendelea katika taifa hili tufate yale rais wetu anayosema kila siku kwamba tusihangaike na mtu ambaye ameshasonga mbele, tuhangaike na mtu ambaye anataka kusonga mbele, mwananchi wa kawaida”Mh. Zelote alisema.
Nae Mkurugenzi wa AMDT Martin Mgala amesema kuwa mikoa ya Rukwa, Songwe, Katavi na Mbeya ni miongoni mwa mikoa 12 ya Tanzania nzima iliyochaguliwa kwenye mpango wa kuhamasisha uzalishaji wa zao la alizeti na kuongeza kuwa kazi iliyopo ni kuwahakikishia wakulima wanauza katika bei nzuri bila ya kupitia kwa watu kati kati.
"Nataka kuwakikishia kwamba kila tunachokifanya kinaendana na mipango ya serikali hatutaki kufanya mambo ambayo yanakwenda kinyume na serikali, hivyo lengo letu ni kuwawezesha wakulima kuuza mazao kwa kuyaongezea thamani, kuzalisha mafuta kwa wingi ili kuondokana na kuagiza mafuta haya kutoka nje ya nchi," Mgala alisema.
Kwa upande wake mgeni rasmi wa mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Songwe Lt. Mstaafu Chiku Galawa amewasisitiza watumishi kufanya kazi kwa umoja kuanzia kwa maafisa ugani hadi kwa wakuu wa idara na kusisitiza kuwa Hakuna anayemiliki miradi na kuwa miradi yote ni ya serikali.
“Utamkuta afisa ugani anasema mradi huo haunihusu unasimamiwa na Fulani, tukimkuta kama huyo tutamshughulikia na wakulima wanakijiji wote mkikutana na afisa ambaye hatoi ushirikiano kwenye miradi ya serikali badi nyie tupigieni simu ili tumshughulikie, haiwezekani alipwe mshahara halafu asifanye kazi, wakati wote anavizia posho tu,” Mh. Galawa alisema
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa