Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesisitiza wakandarasi wanaoendelea na ujenzi wa barabara zilizochini ya mradi wa uimarishaji miji katika Manispaa ya Sumbawanga kuwapatia vijana ajira ili waweze kufaidika na utekelezaji wa miradi hiyo.
Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo vijana hao watakuwa na ari ya kuitunzana kuilinda miradi hiyo na kufaidi kipato watakachokipata kutokana na kazi mbalimbali watakazokuwa wakizitekeleza amabzo hazihitaji kisomo kikubwa kutekeleza.
“Fedha za miundombinu katika Manispaa yetu ni Bilioni 18, sasa zimewafikia ninyi wananchi kwa shuilingi ngapi? Pamoja na kwamba kuna mitambo hiyo inaendelea lakini kuna kazi ambazo lazima vijana waajiriwe, na sisi tutawasimamia kuhakikisha ya kwamba huu mradi unawanufaisha mnapata ajira, na kina mama pamoja na kwamba kuna kazi hizi za barabara lakini kuna kutayarisha chakula kwa hawa wanaofanya kazi za barabara,” Alisema.
Alisema maneno hayo alipotembelea utekelezaji wa program ya uimarishaji miji (ULGSP) unaosimamiwa na OR – TAMISEMI na kufadhiliwa na Benki ya Dunia kwa zaidi ya shilingi bilioni 23 inayojumuisha miundombinu, mifumo ya utendaji, usimamizi wa masuala ya kimazingira, kuimarisha mifumo ya kifedha na kuboresha upimaji katika mipango ya matumizi bora ya ardhi mijini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manaipaa ya Sumbawanga Hamid Njovu amesema kuwa kwa ujumla program hiyo itatengeneza Kilometa 11.5 za barabara za lami katika mji wa Sumbawanga kwa kiwango cha “asphalt concrete” na kuahidi kuwa hadi ifikapo mwezi wa tisa mwaka huu miradi hiyo itakuwa imekamilika.
Mmoja wa wananchi waliokuwepo kwenye eneo hilo Barnabas Juakali ametoa shukrani zake kwa serikali ya awamu ya tano kwa kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi na kumshukuru Rais Dkt. John Pombe magufuli kwa kutekeleza yale yote aliyoyaahidi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa