Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaasa wananchi kuhakikisha wanaimarisha nyumba zao kwa kutumia saruji wakati wa ujenzi wa nyumba hizo na kuepuka kutumia miti aina ya mihama wakati wa kuezeka ili kutoruhusu upepo kuezua na kubomoa nyumba hizo wakati huu ambapo mvua zinaendelea kunyesha maeneo mbalimbali ya mkoa.
Mh. Wanagabo amesema kuwa katika tathmini yake ameona nyumba nyingi zinazojengwa kwa matofali ya kuchoma yanashikizwa kwa tope kuanzia kwenye msingi wa nyumba na hazina lint ana zenye linta hazina makoa na mbaya Zaidi miti aina ya mihama inatumika kuezekea, miti ambayo huwa ni mizuri ikiwa mibichi na endapo ikikauka haiwezi kusaidia misumari kuendelea kushikilia pindi upepo mkali unapotokea.
“Mfuko mmoja (wa saruji) unaweza ukazunguka msingi, tayari ukawa umeimarisha nyumba yako, heri kuzuia kuliko kuponya, kwasababu nyumba inaweza kuanguka na waliomo wakafariki pia, au wanaweza wakapata majeruhi, sasa wale waliofariki utawarudisha, yule majeruhi unajua atapona lini, kisa umeshindwa kuchapia kwa 20,000/=, sasa tupime uzito ni afadhali nyumba yako ukaichapia na Saruji, mchanga unapatikana, saruji inapatikana, kwahiyo msingi ndio nyumba,”
“lakini pia zile mbao mnazoezekea, za hii miti mihama, ile mihama ukiwa mbichi ukipiga msumari unashika vizuri sana, lakini ikishakauka inakuwa na hali ya kutanuka, inaacha nafasi inatanuka, upepo ukija unatoa, tena kiurahisi kabisa, lakini angalieni namna bora ya kuezeka nyumba zenu, na mziezeke kwa mbao, najua huku kuna mchwa, pakeni hata oili chafu na dawa za mchwa halafu unapiga kenchi zako unaezeka lakini hii mihama ndio inayotufikisha hapa,” Alisisitiza.
Aidha, Mh. Wangabo amewasisitiza Maafisa tarafa, Watendaji wa Vijiji na Kata kuhakikisha wanasimamia agizo la kila nyumba kuwa na walau miti minne ili kuweza kuzuia upepo usiweze kuathiri nyumba hizo na hivyo kusaidia kupunguza athari ambazo zinaweza kusababishwa na upepo huo mkali katika makazi ya watu.
Mh. Wangabo ameyasema hayo tarehe 6.3.2021 alipotembelea vijiji vinne vya Mkusi, Kapenta, Kawila na Kaoze, katika Bonde la ziwa Rukwa vilivyopatwa na janga la nyumba 56 kubomolewa na nyumba 26 kuezuliwa na upepo mkali, ambapo katika ziara yake hiyo aliambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa Pamoja na watalaamu wengine.
Wakati akitoa taarifa fupi juu ya tukio hilo Mtendaji wa Kata ya Kapenta Brown Juma alisema kuwa Pamoja na upepo huo kuathiri nyumba Pamoja na miti lakini hakukuwa na majeruhi wa vifo.
Halikadhalika Makam Kwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mh. Apolinary Macheta alipokuwa akielezea matukio kadhaa ya upepo huo mkali yaliyotokea ndani ya miezi miwili, alimuomba Mkuu huyo wa Mkoa kutuma wataalamu ili kuchunguza matukio hayo huku akiwasisitiza wananchi kuendelea kupanda miti ili kujikinga na majanga hayo.
“Sehemu zote ambazo kimbunga kimetokea, maeneo ambayo nyumba zimesalimika ni zile tu ambazo zimezungukwa na miti, eneo lililowazi hakuna nyumba ambayo imesalimika, nishukuru tupo hapa, maeneo mengine Zaidi ya nyumba 200 kama (kijiji cha) Muze, ni kwakuwa eneo lile lilikuwa wazi, naona yawezekana maeneo haya ambayo miti ipo naona kidogo kuna majengo yamesalimika hili ni darasa tosha kuwa mirti inatusaidia,” Alisema.
Godfrey Siwale ni mmoja wa waathiriwa wa kimbunga hicho ambacho kilitokea saa nne asubuhi wakati akiwa shambani huku familia yake ikibaki nyumbani na kusema kuwa upepo huo ulitokea mlimani kushuka bondeni na hatimae kuingia ndani ya nyumba yake na kuinua paa la nyumba hiyo na kulitupa pembeni na hivi sasa anajihifadhi katika nyumba ya jirani.
Aidha, wakati akielezea tukio hilo lilivyotokea Mwenyekiti wa Kijiji cha Kawila, Ruben Masua alisema kuwa upepo huo ulidumu kwa muda wa saa nne kuanzi saa nne asubuhi hadi saa nane mchana ambapo watu wengi walikimbia makazi yao ili kujiokoa na hali hiyo.
“Upepo umekatika muda wa saa nane kasoro, tukaingia kijijini kwakweli, tukakuta kuna nyumba zimeharibika, zimeanguka nyumba kama 45 hivi kwahiyo tulianza kuokoa vyombo, wengine vyombo vilivunjika, meza, masufuria, masinki yamekwisha, kwahiyo ikabidi tuazne nyumba hadi nyumba kuokoa vyombo,” Alisimulia.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa