Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa miezi mitatu kwa wananchi wanaoishi katika kambi ya uvuvi ya Nankanga iliyopo kando ya ziwa Rukwa kuhama kwa hiyari baada ya kambi hiyo kuwa katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kipindupindu kwa kutokuwa na vyoo.
Mh. Wangabo amesema kuwa kuondoka huko kwa hiari kuwepo ndani ya mwezi huu wa kwanza hadi wa nne baada ya kuona wingi wa wananchi wanaoishi katika kambi hiyo pamoja na kutokuwepo kwa kipindupindu kwa wakati huu ila zoezi hilo ni la tahadhari ili kujikinga na ugonjwa huo.
“Hatuwezi kuendelea kuishi mahali hapa ambapo vyoo vyenyewe vinaingiliana na maji ya kunywa, na ili kisije hapa kipindupindu ni lazima watu wasifanye shughuli kwenye ziwa ili kuwe salama, lakini mkiruhusu kipindupindu kuingia hapa tutawafurusha, tena tutawasimamia kweli kweli, tutawapiga quarantine (kuwaweka kwenye kizuizi) mkipona tutawaswaga,” Amesisitiza
Ameyasema hayo alipofanya ziara kwenye kambi ya Nankanga iliyopo katika Kijiji cha Solola Wilayani Sumbawanga ili kujionea hali halisi ya maisha ya wavuvi katika kambi zisizo rasmi na namna ya kuweka mpango salama wa kuweza kuwaepusha na ugonjwa wa kipindupindu ulioenea katika makambi hayo yanayozunguka ziwa Rukwa.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalfan Haule alitoa hadi tarehe 1/5/2018 wananchi hao wawe wameyahama makazi hayo na kujisogeza kwenye vitongoji vya jirani huku akiwasihi viongozi wa vijiji na vitongoji hivyo kushirikiana kuhakikisha wanatoa maeneo kwaajili ya wananchi hao kuhamia.
“Kuanzia tarehe 1 mwezi wa 5 hapa hatutaki kumuona mtu, kama una kibanda chako ama bati lako anza sasa hivi kwa kushirikiana na mwenyekiti wa Kijiji na Mtendaji wa Kata mtafute nafasi katika kitongoji cha Isanga kila mtu ajenge nyumba,” Alisisitiza.
Hatua hiyo imekuja baada ya ugonjwa wa kipindupindu kusambaa kwenye kambi kadhaa za wavuvi pembezoni mwa ziwa rukwa na kusababisha watu 210 kuumwa ugonjwa huo na watu nane kupoteza maisha, ambapo hadi sasa kambi zisizo rasmi zaidi ya tisa zimefungwa huku zoezi hilo likitegemewa kuendelea hadi hapo Mwezi wa tano.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa