WANAFUNZI wapatao 15,193 sawa na asilimia 73, ambao wamefaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na 10,250 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule mbalimbali za sekondari mkoani Rukwa.
Ofisa elimu mkoa wa Rukwa, Nestory Mloka alisema hayo wakati wa kikao cha kutangaza matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu na uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Mloka alisema kuwa kati ya wanafunzi hao 15,193 wavulana ni 7,545 na wasichana ni 7,648 kati ya watahiniwa 21,295 waliosajiliwa kufanya mtihani huo sawa na asilimia 82.19 ya walioandikishwa.
Alisema watahiniwa 482 sawa na asilimia 2.26 hawakuweza kufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za utoro na magonjwa.
Alisema kwamba kutokana na ufaulu huo mkoa umepanda kwa asilimia 4.95 ambao ni 73 ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2017 ambao ulikuwa asilimia 68.05 huku Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ikiongoza kwa wastani wa asilimia 83.40 ikifuatiwa Manispaa ya Sumbawanga, Kalambo na Sumbawanga vijijini ikiburuza mkia.
“Idadi ya wanafunzi wanaotakiwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2019 imeongezeka. Jumla ya wanafunzi 4,943 sawa na asilimia 32.53 hawajachaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kwa mwaka 2019 kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa na hivyo kusubiri chaguo la pili.” Alisema.
Naye, Kaimu Katibu tawala wa mkoa huo, Winnie Kijazi alisema licha ya ufaulu kuonyesha umepanda kwa asilimia nne, bado wadau wa elimu hawapaswi kujivunia kwa kuwa mkoa huo umeporomoka kutoka nafasi ya 15 mwaka 2017 hadi 18 mwaka 2018.
Kijazi alielekeza kuwa ni jukumu la kila Halmashauri kuweka mpango kazi na mpango mkakati wa kufikia asilimia lengwa kwa mujibu wa mwongozo wa matokeo makubwa sasa (BRN) na kuongeza kuwa miongoni mwa mikakati itakayowekwa ni pamoja na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa ufundishaji na ujifunzaji shuleni na kudhibiti utoro wa wanafunzi katika shule.
Hata hivyo mkoa umeendelea kupandisha ufaulu mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2015 asilimia 55.25, mwaka 2016 asilimia 66, mwaka 2017 asilimia 68.05 na mwaka 2018 asilimia 73.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa