Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wanagbo amewaomba wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kuipokea timu ya Tanzania Prisons itakapowasili rasmi mjini sumbawanga leo tarehe 21.8.2020 kwaajili ya kuweka makazi na kuanza maandalizi ya mashindano ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Pia amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini Kamishna Jenerali Selemani Mzee kwa kuridhia timu hiyo kuhamia katika mji wa Sumbawanga, baada ya uongozi wa mkoa kufanya mazungumzo nae na hivyo kuchukua nafasi hiyo kuthibisha taarifa za timu hiyo kuhamia Mkoani Rukwa.
"Hali kadhalika nawaomba Wananchi wa Mkoa wa Rukwa kutoa Michango yao ya hali na mali ya kuiwezesha Timu hiyo kuweka Makazi yao ya kudumu hapa Sumbawanga na pia kuwezesha gharama za Maandalizi."
Mh. Wangabo aliitaja Akaunti namba ambayo wananchi wanatakiwa kuichangia timu hiyo ili kuweza kuendelea na maandalizi ya Ligi kuwa ni 9921169733 jina la Akaunti RUKWA SUB TREASURY MISC. DEPOSIT EXP ACCOUNT Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Aidha, Mh. Wangabo alisema kuwa kwa zaidi ya miaka 23 Mkoa wa Rukwa umekosa timu ya mpira wa miguu inayoshiriki mashindano yenye sura ya kitaifa hali ambayo imeathiri maendeleo ya soka katika mkoa nanjari na manufaa mengine ya kiuchumi na kijamii.
Mh. Wangabo aliongeza kuwa ufanisi wa Fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) ulikuwa chachu ya kutafuta timu ya Ligi Kuu ili kuleta furaha kwa wananchi wa Rukwa na Mikoa ya jirani sambamba na kukuza vipaji vya soka pamoja na kuinua hali ya uchumi wa wananchi wa Rukwa kwa ujumla.
Timu hiyo ya Tanzania Prison inatarajia kufungua mchezo wake wa kwanza ugenini ikipambana na timu ya Young Africans katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dare es Salaam tarehe 6 Septemba, 2020 huku mchezo wa kwanza katika Uwanja wa nelson mandela ukitarajiwa kuchezwa tare 19 Septemba 2020.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa