Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wafanyabiashara wa vyakula katika masoko ya Mkoa huo kuwa na moyo wa huruma kwa wale watakaofunga mwezi mtukufu wa Ramadhani kwani ni mwezi wa toba ambao waumini hujinyima kwaajili ya watu wengine.
Amesema kuwa mwezi wa ramadhani ni kipindi ambacho waumini humrudia Mwenyezi Mungu kwa nguvu zote, hivyo sio kipindi cha wafanyabiashara hao kujinufaisha kwa watu wanaofunga, kwani waumini wamekuwa wakijidunduliza ili kusaidia wasiojiweza lakini wafanyabiashara hao wanaona ni fursa ya kujinufaisha.
“Hiki ni Kipindi ambacho wanawasaidia watu mbalimbali kwa nguvu zao zote, sasa akamsaidie mtu mwingine na wakati huo huo akusaidie wewe ambaye unataka kujinufaisha kwa manufaa yako mwenyewe ukijua kabisa kwamba hiki ni kipindi maalum cha kumrudia Mwenyezi Mungu niwasihi sana wafanyabiashara wote msiongeze bei ya vyakula mbalimbali ten asana sana mshushe bei za vyakula, nisinikie bei zimepanda sijui ongezeko la bei ya sukari sijui ya unga, maharage sitaki kusikia nataka kusikia bei zimeshuka, “ Alisisitiza.
Aidha, amewatakia mfungo mwema wa mwezi wa Ramadhani Waislamu wote Tanzania pamoja na wale waumini wa dini mbalimbali watakaosindikiza mwezi huo na kumuomba Mwenyezi Mungu atupe baraka kutokana na mwezi huo ndani ya Mkoa wa rukwa na Tanzania kwa ujumla.
Waislamu wote wa Tanzania wanatarajia kuungana na waislamu wengine duniani kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani huku waumini wa Tanzania wakianza kufunga kuanzia tarehe 7.5.2019.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa