Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka watendaji wa vijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuhakikisha hadi kufikia mwishoni mwa mwezi wa pili wakamilishe zoezi la kuwatambua wajasiliamali waliopo kwenye maeneo yao, kuwasajili pamoja na kuwapa vitambulisho na kuahidi kupita Kijiji hadi Kijiji kuona kuwa zoezi hilo linafanikiwa kwa ukamilifu.
Mh. Wangabo amewaonya watendaji hao wa vijiji 112 kuwa mwananchi wa Kijiji chochote atakayebainika kuendelea kufanya biashara hali ya kuwa hana kitambulisho Mtendaji wa Kijiji hicho atakuwa maekwenda kinyume na maagizo na hivyo kuwa matatani na kuongeza kuwa wigo wa walipa kodi kwa mkoa wa Rukwa ni mdogo mno hivyo kulinganisha na mahitaji yaliyopo ndani ya mkoa na hivyo kuwataka wajasiliamali wote kuona umuhimu wa kuwa na kitambulisho hicho ili kutambulika na serikali kama mfanyabiashara mdogo.
“Pale mheshimiwa rais aliposema wafanyabiashara ndogondogo wasibughudhiwe alikuwa na maana kwamba ni lazima wawe na vitambulisho, kwamba wewe hustahili kulipa kodi ya TRA, sasa wewe hulipi kodi ya TRA nah una kitambulisho kinachokujulisha kwamba wewe ni mfanyabiashara mdogomdogo, sasa wewe uko wapi, uko ndani ya nchi hii ama wewe ni Mkongo au Mzambia, sasa baada yah apo itabidi usumbuliwe na tutakusumbua,” Alinaisha Mh. Wangabo.
Ameyasema hayo katika kikao kazi kilichowakutanisha watendaji wa Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga katika Kijiji cha Mtowisa, Kata ya Mtowisa ili kuzungumzia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya tano katika Halmashauri hiyo pamoja na kuwakumbusha majukumu yao kama wawakilishi wa serikali katika ngazi ya Kijiji.
Akielezea utaratibu wa kupata kitambulisho hicho Meneja wa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Rukwa Fredrick Kanyiriri alisema kuwa kabla ya kupewa kitambulisho ni lazima ujaze fomu ambazo zinapatikana kwa watendaji wa kata pamoja na watendaji wa vijiji na mitaa ndipo uweze kupatiwa kitambulisho hicho baada ya kulipia shilingi 20,000/= na kuongeza kuwa fomu hizo ni bure ila ukibainika kuwa umeidanganya serikali hatua za kisheria lazima zichukuliwe.
“Kikubwa ni kuhakikisha kuwa huyo mtu aidha ana TIN kwa maana ya kwamba analipa kodi ya TRA na kama hana TIN basi mtu huyo anatakiwa apatiwe kitambulisho, pia mnaweza kukutana na wengine waliotutoroka, mtu anaweza akakwambia kuwa mimi nalipa kodi ya mapato ni lazima akuthibitishie, atakuwa na ile TIN na risiti yake,” Alifafanua.
Akieleza makundi yanayostahili kupatiwa vitambulisho hivyo Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule amewata kuwa ni waendesha bodaboda, wauza mafuta petrol vijijini, wauza pombe za kienyeji, mama ntilie, wauza matunda, waziba pancha za baiskeli, wauza nyanya na mboga mboga, wachinjaji wa mifugo pamoja na wale wote wanaofanya biashara ambayo mapato ghafi hayajafikia shilingi milioni nne kwa mwaka.
Aliongeza kuwa kwenye fomu hizo za kujaza kabla ya kupewa kitambulisho kuna sehemu ya picha hivyo picha hiyo si muhimu kwani kitambulisho hicho kina namba tu na hakina picha hivyo mjasilimali kama atakuwa amesahau kitambulisho hicho anachotakiwa kufanya ni kukariri namba ya kitambulisho hicho pindi atakapoulizwa ili asibughudhiwe.
Waliosajiliwa kulipa kodi ya mapato katika Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa Mkoa mzima wa Rukwa ni 18,199 kati hao walipa kodi 7,787 hawalipi na hivyo kubakiwa na walipa kodi 10,412 kati ya wananchi zaidi ya milioni 1.2 wa Mkoa wa Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa