Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatahadharisha wananchi juu ya kuingilia Mhimili wa mahakama baada ya kupokea malalamiko ya wakulima 112 waliouza tani 622 za mahindi kwa chama cha ushirika cha mazao MUZIA AMCOS bila ya kulipwa fedha zao kwa msimu wa 2016/2017 ambapo kesi hiyo ipo mahakamani na kutegemewa kusikilizwa tarehe 27/2/2018.
Wananachi hao wanaokidai chama hicho Shilingi Milioni 315 wameiomba serikali kuchukua mzigo huo wa deni baada ya chama hicho kutoa ahadi kadhaa za malipo tangu tarehe 10/10/2017 na kushindwa kulipa na kupelekea wananchi hao kushindwa kujiendeleza kiuchumi.
Amesema kuwa haingilii mahakama pale anaposikiliza kero za wananchi isipokuwa kesi ikiwa mahakamani hana mamlaka ya kumlazimisha Jaji cha kufanya kwani mahakama zinataratibu zao za kuendesha kesi na kuwasihi wakulima kusubiri hukumu ya kesi hiyo ndipo aweze kushughulikia na kuwahakikisha kupata haki yao pindi hukumu itakapotoka.
“Tumeambiwa hapa kuwa hilo suala ltasikilizwa tarehe 27/2/2018, sasa hebu tusubili tuone ile hukumu itatoka na itakuwa ya namna gani kwahiyo siwezi kuisemea, nikiisemea inamaana nitakuwa naingilia uhuru wa mahakama, tusubiri tusikie hukumu itasemaje juu ya kuipata hiyo fedha milioni 315, wakulima watapataje na mhukumiwa atapewa adhabu gani, ikishatoka ndipo serikali tutajua tufanye kitu gani,” Alisisitiza.
Awali akisoma risala fupi kwa niaba ya mrajisi wa vyama vya ushirikia Mkoa wa Rukwa Nicolas Mrango alisema kuwa baada ya kubaini kasoro kadhaa katika chama hicho waliitisha kikao cha bodi na wajumbe wa bodi hiyo walielekeza lawama kwa Mwenyekiti na katibu wa chama hicho na kupelekea viongozi hao kufikishwa polisi na hatiame kesi kufikishwa mahakamani.
“Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuwasimamisha uongozi viongozi waliotuhumiwa kuhusika na upotevu wa mahindi ya wakulima ili kupisha vyombo vya uchunguzi kutekeleza majukumu yake pasipo kuingiliwa,” Alisema.
Nae katibu wa wakulima kata ya Mambwekenya Geofrey Siyame aliitaka serikali kuchukua mzigo wa deni kwakuwa serikali ndio iliyotoa uwakala wa kununua mahindi ya wakulima kwa chama hicho na kueleza kuwa hadi sasa wameshindwa kununua pembejeo ili kuendelea na shughuli za kilimo na kuwa hawana Imani na mahakama.
“Tumepata taarifa kwamba serikali imepeleka madai mahakamani, mahakama imekuwa ikirusha tarehe kile kesi inapotanjwa kwa madai upelelezi unaendelea, kwanininuchunguzi unachukua muda mrefu, wakulima mpaka sasa hawana Imani na mahakama baada ya kutishiwa na mdaiwa kuwa anadili na mahakama,” Alisema.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa