Viongozi wa kanisa la Free Pentecostal Church of Tanzania wakiongozwa na Askofu Julius Mwanakatwe wametoa msaada wa mahindi kilo 500 na fedha taslimu shilingi 100,000/= kwaajili ya waathirika wa mvua zilizoathiri nyumba zaidi ya 300 katika maeneo kadhaa ya Mkoa wa Rukwa.
Kanisa hilo limetoa msaada baada ya kuguswa na kilichotokea kwa wanafamilia hao waliopoteza makazi ya kuishi kutokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha mwishoni mwa mwaka 2018 katika maeneo ya kipeta na Kilyamatundu katika bonde la ziwa Rukwa pamoja na maeneo ya wilaya ya Nkasi.“Zawadi hii tuliyoitoa ni kidogo, fedha hizi pamoja na mahindi tunaamini yatasaidia,” Alisema Askofu Mwanakatwe.
Wakati akipokea msaada huo Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alitoa shukrani kwa niaba ya serikali ya mkoa na kuwaomba viongozi wengine wa madhehebu ya dini kuonesha ushirikiano katika kipindi hiki cha kuwafariji waathirika hao.
“Huu ni moyo wa huruma ambao mnao viongozi wa kanisa, nitumie pia fursa hii kutoa rai na wito kwa viongozi wengine wa madhehebu ya dini kwamba tunapokuwa na majanga kama haya basi tuendelee kushirikiana namna hii na hivi ndivyo tutaufanya mkoa wetu uendelee na ushirikiano,” Alisema.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa