Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mh. Queen Cuthbert Sendiga amekabidhi misaada ya kiutu kwa kwa wahanga wa mafuriko yaliyotokea mapema mwezi Aprili 2023 katika Kata ya Mfinga Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Misaada ilivyokabidhiwa ni pamoja na Maharage kilo 1120, unga wa sembe kilo 1440, Mafuta ya kupikia lita 154, mikeka, vyandarua, mablanketi seti za masufuria na miche 250 ya miti ili kusaidia kurejesha uoto katika maeneo yaliyoathirika.
Akikabidhi misaada hiyo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ameagiza mgawanyo wa misaada hiyo uzingatie mahitaji na wakati wa ugawaji kipaumbele wapewe watoto, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha.
Kiongozi huyo wa Mkoa ameitaka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutafuta dawa kwa ajili ya kutibu maji baada ya kupokea maombi ya wakaazi wa vijiji hivyo vilivyoathiriwa na mafuriko. Amemwelekeza Meneja wa Mamlaka hiyo Wilayani Sumbawanga kuhakikisha maji ya visima vilivyopo yanatibiwa ili wananchi wapate maji safi na salama kwa haraka wakati mradi mkubwa wa maji unaoendelea kutekelezwa kwa awamu ukiendelea.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amewaagiza wananchi wa Kijiji cha Msila, Kasekela na wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa kuondoka na kuacha kulima kandokando ya mito kwa hiyari yao wenyewe kabla ya kuondolewa kwa shuruti. Amewaambia wananchi hao kuwa mafuriko na mabadiliko ya tabia nchi yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanyika kandokando ya mito, milimani na katika vyanzo vya maji na maeneo mengine.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa