Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza mkuu wa Wilaya ya Nkasi kuhakikisha anawatumia watendaji wa kata na vijiji pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kuhakikisha wanawasaka na kuwakamata wanafunzi watoro pamoja na wazazi waoili kuhakikisha wanafunzi wote wanafika shule.
Amesema kuwa kwa kufanya hivyo itakuwa fundisho kwa wazazi ambao kwa makusudi wanaacha watoto wao kutokwenda shule huku akipigia mfano faida ya elimu kwa kuwataja viongozi mbalimbali wa kiserikali akiwemo yeye mwenyewe pamoja na wataalamu waliozingatia elimu na matokeo yake wamefanikiwa kimaisha.
“Kuna wanafunzi 173 watoro, hawajafika shuleni, sasa Mkurugenzi fuatilia shule yako, mkuu wa wilaya tumia watendaji wa vijiji, wa kata, kamati yako ya ulinzi, sakeni wanafunzi wote kamateni wazazi wao mpaka walete watoto wao shule, hatubembelezani hapa,”Alibainisha.
Ameyasema hayo alipotembelea shule ya sekondari Korongwe Beach katika Kijiji cha korongwe, kata ya Korongwe Wilayani Nkasi ili kujionea mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza pamoja na ujenzi wa madarasa ambapo wanafunzi 50 wamepangiwa kuanza kidato cha kwanza huku 17 tu wakiwa wameripoti na shule ikiwa na jumla ya wanafunzi 383.
Awali akitoa taarifa ya shule hiyo Mwalimu Mkuu wa shule Nicomedi Ntepele amezitaja changamoto za shule hiyo ikiwemo utorowa rejareja na wa kudumu, ukosefu wa madarasa na nyumba za waalimu, ofisi za waalimu na maji.
“miongoni mwa changamoto tulizonazo hapa shule ni pamoja na utoro wa wanafunzi wa reja reja na wa kudumu, ukosefu wa madarasa, pia wazazi kutokuwa na uelewa kuwaleta Watoto wao kuishi hostel, uhaba wa maji eneo la shule, ofisi za walimu kutokamilika hivyo tunaomba changamoto hizi kufanyiwa kazi ili tufanye kazi kwa ufanisi,” Alimalizia.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Missana Kwangula aliamua kubadilia matumizi ya hosteli ya wanafunzi wa kike kutumiwa na wanafunzi wa kiume baada ya Mh. Wangabo kumtaka ajibu maombi ya mwanafunzi Ibrahimu Musa ambaye pia ni kaka mkuu wa shule hiyo juu ya kujengewa hosteli baada ya Mkuu wa Mkoa kutoa nafasi kwa wanafunzi kuuliza maswali.
“Wanafunzi tunatembea umbali mrefu hasa Watoto wa jinsia ya kiume, sisi tulikuwa tunaomba ndugu Mkuu wa Mkoa uweze kutujengea sisi pia hosteli ili na sisi tuweze kukaa bweni nasi tuweze kufanya vizuri katika masomo yetu,”Alisema
Katika shule hiyo ya Korongwe Beach Sekondari kuna hosteli ya wanawake iliyojengwa kwa msaada wa watu wa Japan (JAICA) pamoja na serikali ya Tanzania, hosteli ambayo kwa mujibu wa taarifa ya mwalimu mkuu wa shule haijawahi kutumika tangu kumaliziwa kwake, ndipo Mkurugenzi aliposema.
“Hosteli ile ilipojengwa ilikuwa ni kwaajili ya kuawasaidia Watoto wa kike kwasababu ndio wanachangamoto zaidi, lakini kwasababu hosteli ile hawaingii walengwa ambao wako hapa, tuna uwezo tu wa kuibadilisha matumizi na uiandika hosteli ya wavulana kuliko kujenga hosteli nyingine, tutakapobadili matumizi ninyi Watoto wa kike msige kuidai tena wakati ipo sasa hamuingii,” Alimalizia.
Shule ya Sekondari Korongwe Beach ina wanafunzi 383 na kushika nafasi ya kwanza kiwilaya katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2018. Na wanafunzi 50 wamepangwa kuanza kidato cha kwanza huku 17 wakiwa wameripoti shuleni.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa