Katibu tawala wa Mkoa wa Rukwa Benard Makali amewaasa waandishi wa habari wa mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanatoa elimu sahihi juu ya chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi inayotarajiwa kuzinduliwa katika wiki ya mwisho ya mwezi huu wa nne.
Amesema kuwa wananchi wengi wanaamini zaidi vyombo vya habari hivyo waandishi wa habari wakiandika habari sahihi kuhusu chanjo hiyo itawashawishi wengi kujitokeza kushiriki katika zoezi hilo ambalo nia yake ni kuokoa maisha ya wasichana kwa manufaa ya kizazi hiki na kijacho.
“Lengo kuu la kuwaiteni ni kuomba ushiriki wenu wa hali na mali katika maadalizi na wakati wa utoaji wa chanjo hii muhimu, na kwa kutambua umuhimu wa tasnia hii ya habari, serikali kupitia Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto kwa kushirikiana na wadau wengine wa chanjo nimeona ni vyema wanahabari mkapata fursa ya kupewa elimu ya kutosha kuhusu zoezi hili ili muweze kufikisha ujumbe kwa jamii,” Alisisitiza.
Aliyasema hayo alipokuwa akifungua semina ya siku moja kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Rukwa kuhusu uanzishwaji wa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi katika mkoa iliyofanyika katika ukumbi wa hospitali ya rufaa ya mkoa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa Mkoa wa Rukwa Musa Mwangoka amesema kuwa mafunzo hayo yamewasaidia katika kulielewa zoezi hilo linaloendelea kwa kina na kuahidi kutoa ushirikiano katika kufikisha ujumbe kwa jamii ili kuokoa maisha ya wasichana hao.
Aidha mwakilishi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI anayetokea katika idara ya afya ya wizara hiyo Nkinda Shekalaghe amesema kuwa waandishi wa habari wakipata taarifa sahihi nao huzifikisha katika jamii katika usahihi ule ule uliokusudiwa na watakaopokea taarifa watapokea kwa usahihi na zilizo kamili.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa