Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema hatamvumilia mtendaji wa serikali atakaechangia kuenea kwa ugonjwa kipindupindu katika mkoa kwani elimu ya ugonjwa huo imeshatolewa kwa muda mrefu hivyo ni jukumu la kila mtendaji kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa.
Amesema kuwa kumekuwa na tabia iliyojengeka ya watendaji kuanza kufanya majukumu yao baada ya mlipuko wa ugonjwa huo kutokea na kuonya kuwa kaya ambayo haitakuwa na choo katika ngazi ya Kijiji basi mtendaji wa Kijiji atawajibishwa.
“Wakati hatua mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa, tukikidhibiti kipindupindu halafu kikatokea tena hapo mahali ambapo kimetokea hatutapaelewa, watendaji wetu wakitilia maanani wakahakikisha kaya zetu zina vyoo na kuchemsha maji hatuwezi kuwa na kipindupindu, sasa kinatokea kipindupindu halafu kaya haina choo, mtendaji wa Kijiji hicho hana sababu ya kuwa mtendaji,” Alisisitiza.
Ameyasema hayo alipokuwa akifunga kikao cha dharura kilichoitishwa na kamati ya afya ya mkoa ili kujadiliana juu ya mbinu za kutokomeza ugonjwa huo ambao umeathiri zaidi ya watu 600 tangu kulipukwa kwake mwezi November mwaka 2017 na kutoweka mwezi Machi mwaka 2018 na hatimae kuibuka tena tarehe 6, Mei mwaka 2018.
Kikao hicho kilichojumuisha, Wakuu wa ilaya, Wakurugenzi wa halmashauri, Wenyeviti wa halmashauri, madiwani, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na wilaya, Maafisa Afya wa mkoa na halmashauri, wataalamu wa afya pamoja na waganga wakuu wa wilaya na mganga mkuu wa mkoa kiliazimia kutokomeza ugonjwa huo na kuweka mikakati ya kutorejea tena wa ugonjwa huo.
Akisoma baadhi ya maazimio Katibu Tawala wa Mkoa Benard makali amesema kuwa kamati ya afya za vijiji na vitongoji zisimamiwe kutenda majukumu yake kwani wao ndio wanaojuana zaidi katika utekelezaji wa maagizo na sheria za serikali kuanzia ngazi hizo na kuitaka kamati za afya za Wilaya kuwa na mbinu za kudumu za kuthibiti ugonjwa huo na kutaka elimu zaidi iendelee kutolewa.
Tangu kulipuka tena kwa ugonjwa huo tarehe 6, Mei mwaka 2018 wagonjwa 9 wamefariki na wengine 214 wakiendelea kupatiwa matibabu katika vituo mbalimbali vya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ambayo imeathirika zaidi huku wananchi wake wakiwa na asilimia 36 ya umiliki wa vyoo bora.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa