Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi Dkt Angeline Mabula alisema, wizara yake imeridhia kuanzishwa Baraza la Ardhi la Nyumba la wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
Hatua hiyo inafuatia Dkt Mabula kuridhishwa na juhudi za wilaya ya Nkasi katika kuanzisha baraza hilo ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi yake katika makao makuu ya Wilaya hiyo mjini Namanyere na kusema kuwa kwa sasa takriban mabaraza 100 ya ardhi na nyumba ya wilaya yameidhinishwa lakini ni mabaraza 55 tu ndiyo yanayofanya kazi.
Hata hivyo, aliongeza kuwa, wakati mchakato wa ofisi za baraza hilo ukiendelea Mwenyekiti wa baraza la ardhi la wilaya ya Sumbawanga anaweza kupanga ratiba na kwenda kuendesha mashauri ya migogoro ya ardhi kwenye wilaya ya Nkasi kwa lengo la kupunguza mashauri hao.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa, mkoa wake una baraza moja tu la ardhi la nyumba na wilaya huku mkoa mzima ukiwa umesajili jumla ya mashauri 308 ya migogoro ya ardhi kuanzia mwezi januari hadi juni mwaka huu.
Alisema, kufuatia hali hiyo iko haja ya kuanzishwa baraza la ardhi la wilaya ya Nkasi kwa kuwa wananchi wa wilaya hiyo wamekuwa wakipata taabu kutembea umbali mrefu na wakati mwingine hulazimika kusafiri zaidi ya kilomita 200 kufuata huduma ya baraza wilayani Sumbawanga.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa