Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaonya vikali wenyeviti wa vijiji wananojihusisha na kuwajazia watu wasio raia wa Tanzania fomu za mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA) ili kuhalalisha uwepo wao katika nchi na kuongeza kuwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa sheria.
Pia aliwaasa wananchi kuwa macho na wale wanaopewa fomu hizo hali ya kuwa sio raia na hawastahili kupewa vitambulisho hivyo na kuwasisitiza kuwa walinzi wa kwanza wa taifa la Tanzania ili wananchi ambao ni raia wa Tanzania wanaostahili kupata fomu hizo ndio wapatiwe.
“Mwenyekiti yoyote wa Kijiji akibainika amemwandikisha mtu amabae sio raia, ambae hastahili na hana vibali husika vinavyomruhusu apate kitambulisho cha taifa, ukibainika tunakukamata tunakuweka ndani, halafu tunakufungulia mashataka kwasababu utakuwa msaliti na unalisaliti taifa letu, na nyie wananchi ndio macho yetu yeyote mnaeona sio raia na amepewa fomu muwekeeni kipingamizi, kwasababu sheria inaruhu,” Alisema.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha mtowisa, kata ya mtowisa, wilayani Sumbawanga alipokwenda kutemebelea na kuijionea miradi kadhaa ya kimaendeleo inayoendelea kutolewa katika ukanda wa bonde la ziwa Rukwa.
Kwa upande wake Mratibu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya taifa (NIDA)Mkoani Rukwa Emanuel Mjuni amesema kuwa katika kata ya Mtowisa wanatarajia kuwaandikisha wananchi 5,430 na kusisistiza kuwa wale wasiokuwa wakazi wa kata hiyo hawana vigezo vya kupata fomu na hatimae kukosa vigezo vya kupata vitambulisho hivyo vya taifa.
“Kama tukiwaandikisha wananchi ambao hawaishi kwenye maeneo yetu wale wananchi ambaotumewaandalia fomu hizo watakosa, kama Mh. Mkuu wa Mkoa alivyosema wale wenyeviti na watendaji wa vijiji wasimamie kwa makini kuhakikisha yule anaepata fomu ni mkazi halali wa eneo husika na zoezi hili linafanyika nchi nzima hivyo basi wale ambao wapo huku kibiashara ama kwa mambo mengine warudi kwenye maeneo yao ili waandikishwe, ili wasikose vitambulisho,” Alisisitiza.
Majibu hayo yaliibuka baada ya maswali kadhaa kutoka kwa wananchi Pius Wapinda na Paulo Chipeta waliotaka kujua endapo ni ruhusa kwa wafanyabiashara kuchukua fomu za maombi ya vitambulisho vya taifa katika eneo ambalo zoezi hilo limemkuta ili aweze kuchukua fomu na kupata kitambulisho na hatimae kuwa na utambulisho wa uraia wa nchi yake na pia hatua zitakazochukuliwa kwa wenyeviti watakaokiuka taratibu za kutoa fomu.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa